logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Refa Michael Oliver na familia yake wanapokea vitisho baada ya mechi ya Wolves dhidi ya Arsenal

Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) pia imesema inalaani vikali vitisho na unyanyasaji unaoelekezwa kwa Michael Oliver.

image
na Samuel Mainajournalist

Football27 January 2025 - 07:34

Muhtasari


  • Oliver alimpa mlinzi Myles Lewis-Skelly kadi nyekundu baada ya kumpiga mlinzi Matt Doherty juu ya kifundo cha mguu na kuvunja shambulio la kaunta nje.
  • "Tunamuunga mkono Michael, na wote walioathirika, na tumedhamiria kukabiliana na tabia hii isiyokubalika," taarifa hiyo ilisoma.


Polisi nchini Uingereza wanachunguza madai ya vitisho na unyanyasaji dhidi ya mwamuzi Michael Oliver kufuatia mchezo wa Arsenal dhidi ya Wolves mnamo siku Jumamosi, Bodi ya Waamuzi wa Uingereza (PGMOL) imesema.

Oliver alimpa mlinzi wa Arsenal Myles Lewis-Skelly kadi nyekundu baada ya kumpiga mlinzi Matt Doherty juu ya kifundo cha mguu na kuvunja shambulio la kaunta nje kidogo ya eneo la goli la Wolves kunako dakika ya 43.

Uamuzi huo uliungwa mkono na Darren England, ambaye alikuwa mwamuzi msaidizi wa video (VAR) wa mchezo huo uliochezwa katika uwanja wa Molineux.

Katika taarifa ya Jumapili jioni, siku moja baada ya mechi ambayo Arsenal ilishinda 1-0, PGMOL walieleza kusikitishwa kwao na kile kilichompata Michael Oliver baadaye na kulaani vikali mashambulizi dhidi yake.

"Tumeshtushwa na vitisho na unyanyasaji unaoelekezwa kwa Michael Oliver. Hakuna afisa anayepaswa kudhulumiwa kwa aina yoyote, achilia mbali mashambulizi ya kuchukiza yaliyolenga Michael na familia yake katika muda wa saa 24 zilizopita," ilisema bodi ya waamuzi PGMOL.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa uchunguzi kadhaa umeanza.

"Tunamuunga mkono Michael, na wote walioathirika, na tumedhamiria kukabiliana na tabia hii isiyokubalika," taarifa hiyo ilisoma.

"Cha kusikitisha, hii si mara ya kwanza kwa ofisa wa mechi kulazimika kukabiliana na vitisho katika siku za hivi karibuni. Tutaendelea kuunga mkono uchunguzi wote," iliongeza PGMOL.

Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa upande wake ilisema inalaani vikali vitisho na unyanyasaji unaoelekezwa kwa Michael Oliver.

Hakuna afisa anayepaswa kukabiliwa na aina yoyote ya unyanyasaji. Tutaendelea kumuunga mkono Michael, PGMOL na uchunguzi wote," EPL ilisema katika taarifa.

Wakati wa mechi ya Jumamosi, Oliver pia alimuonyesha kadi nyekundu kiungo wa Wolves Joao Gomes baadaye kwenye mechi kabla ya Riccardo Calafiori kuifungia Arsenal bao la ushindi kwa bao pekee katika mchezo huo.

Baada ya mechi, meneja wa Arsenal Arteta alisema uamuzi wa kumpa kadi nyekundu Lewis-Skelly ulikuwa mbaya sana kwamba hakuhitaji kusema maneno yoyote.

Uamuzi huo pia ulikosolewa na maafisa wa zamani na wachambuzi.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved