
David Coote, mwamuzi aliyepigwa kalamu
katika Ligi ya Premia, amesema mapambano yake ya kijinsia yake yalichangia
maamuzi mabaya ambayo yalimgharimu kazi yake mwaka jana.
Mwamuzi huyo mwenye umri wa miaka 42 alifukuzwa
kazi na bodi ya waamuzi (PGMOL), baada ya kuonekana kwenye video kadhaa za
kutatanisha ambazo zilivuja mtandaoni.
Katika moja ya hizo video, Coote alisikika akimtusi meneja wa zamani wa Liverpool Jürgen Klopp, na katika video nyingine alionekana akivuta unga mweupe.
Katika mahojiano yake ya kwanza tangu kashfa hiyo, Coote hakupinga madai mengi dhidi yake lakini alilaumu masuala ya kibinafsi.
"Nimekuwa na masuala kuhusu kujiamini kwangu - na hiyo inahusiana na jinsia yangu. Mimi ni shoga na nimejitahidi kujivunia kuwa ‘mimi’ kwa muda mrefu,” Coote aliambia gazeti la Sun.
“Nilihisi aibu sana katika miaka yangu ya utineja hasa. Sikufichua kwa wazazi wangu hadi nilipokuwa na umri wa miaka 21. Sikufichua kwa marafiki zangu hadi nilipokuwa na umri wa miaka 25. Ujinsia wangu sio sababu pekee iliyoniongoza kuwa katika nafasi hiyo. Lakini sisemi hadithi ya kweli ikiwa sisemi kwamba mimi ni shoga, na kwamba nimekuwa na mapambano ya kweli kukabiliana na kuficha hilo.”
"Nilificha hisia zangu kama refa mdogo na nilificha jinsia yangu pia - ubora mzuri kama mwamuzi lakini ubora wa kutisha kama mwanadamu. Na hiyo imeniongoza kwenye mwenendo mzima wa tabia,” aliongeza.
Coote alisema pia alihofia kujitokeza kutokana na manyanyaso ambayo angeyapata katika soka kutokana na matokeo hayo.
"Nimepokea unyanyasaji usiopendeza wakati wa kazi yangu kama refa na kuongeza jinsia yangu ingekuwa vigumu sana," alisema.
Msongo wa mawazo wa kuwa refa wa kiwango cha juu ulizidisha shinikizo zaidi na Coote alisema alikuwa anatumia dawa kukwepa shinikizo.
"Sio kitu ambacho nilikuwa nikitegemea siku baada ya siku, wiki baada ya wiki, mwezi kwa mwezi. Nimekuwa na muda mrefu ambapo sijaitumia - lakini ilikuwa mojawapo ya njia za kutoroka niliyokuwa nayo. Kuondoka tu kutoka kwa mafadhaiko, kutochoka kwa kazi. Inanijaza aibu kubwa kusema kwamba nilichukua njia hiyo.”
"Sijitambui kwenye video ya kokeini," Coote aliongeza, akithibitisha unga ambao alionekana akivuta kwenye video alipokuwa akifanya kazi kwenye michuano ya Uropa msimu uliopita kama afisa wa VAR.
"Siwezi kukubaliana na jinsi nilivyohisi wakati huo, lakini ni mimi. Nilikuwa nikipambana na ratiba na hakukuwa na nafasi ya kuacha. Na kwa hivyo nilijikuta katika nafasi hiyo - kutoroka, "aliongeza.
Mwezi Disemba mwaka jana, PGMOL iligundua kuwa kitendo cha Coote kilifanya nafasi yake kama afisa wa Ligi Kuu kuwa 'kutokubalika' na shirika hilo linaloongozwa na Howard Webb lilikatisha kazi yake mara moja.