
Beki
Myles Lewis-Skelly amekwepa kufungiwa mechi tatu baada ya Arsenal kufanikiwa
kukata rufaa dhidi ya kadi yake nyekundu liyoonyeshwa kwenye mechi dhidi ya
Wolves Jumamosi.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 18 alionyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja na mwamuzi Michael Oliver katika kipindi cha kwanza cha mechi hiyo ambayo Arsenal ilishinda 0-1 kwa kumwangusha Matt Doherty katika nusu yao.
Siku ya Jumanne jioni, Shirikisho la Soka la Uingereza(FA) lilithibitisha kuwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 18 hatatumikia marufuku ya mechi tatu.
"Tume huru ya Udhibiti imekubali madai ya kuondolewa uwanjani kimakosa kuhusiana na Myles Lewis-Skelly na kuondoa adhabu yake ya kutocheza mechi tatu," msemaji wa FA alisema katika taarifa.
"Mchezaji huyo wa Arsenal alitolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kucheza vibaya wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu dhidi ya Wolverhampton Wanderers Jumamosi, Januari 25, 2025," taarifa hiyo ilisema zaidi.
Lewis-Skelly amekuwa mchezaji wa tatu mwenye umri mdogo zaidi kutimuliwa katika historia ya Premier League, lakini Wanabunduki walikata rufaa kwa nia ya kutaka kadi hiyo nyekundu kubatilishwa na uamuzi wa FA unamaanisha kuwa beki huyo wa pembeni mwenye uwezo mkubwa hatasimamishwa.
Skelly alionyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja baada ya kumchezea vibaya Matt Doherty, huku mwamuzi Michael Oliver akiona kuwa ni mchezo mchafu mbaya.
Doherty alikuwa nje kidogo ya kisanduku cha Wolves alipopandisha shambulizi la kaunta katika dakika ya 43. Awali uamuzi huo ulikubaliwa na Darren England, ambaye alikuwa mwamuzi msaidizi wa video (VAR).
Wolves baadaye ilishuka hadi wachezaji 10 baada ya Joao Gomes kuonyeshwa kandi ya njano ya pili katika dakika ya 70, kabla ya bao la Riccardo Calafiori dakika ya 74 kuipa Arsenal ushindi wa 1-0.
Mara tu baada ya mchuano wa Jumamosi, Arteta alisema uamuzi huo ulikuwa wazi sana kwamba hakuhitaji kusema chochote.
"Nimekasirika kabisa lakini nawaachia. Kwa sababu ni dhahiri, sidhani kama maneno yangu yatasaidia," Arteta alisema.
Lewis-Skelly sasa yuko tayari kwa mechi ya Arsenal ya nyumbani dhidi ya Manchester City Jumapili, na pia mkondo wa pili wa nusu fainali ya Kombe la Carabao dhidi ya Newcastle mnamo Februari 5, na safari ya Ligi Kuu ya Leicester mnamo Februari 15.
Arteta alijibu habari hizo kwenye mkutano wake na waandishi wa habari kabla ya mchezo wa Wanabunduki wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Girona, akisema: "Ni wazi, nina furaha sana kwamba uamuzi umefanywa na Myles ataweza kucheza tena."
Arteta alipoulizwa jinsi Lewis-Skelly alichukua habari hiyo, Arteta alisema: "Alikuwa amelala kwenye ndege nilipotazama nyuma na nikapata habari, kwa hivyo sijazungumza naye, lakini ninafikiria tabasamu kubwa usoni mwake."