logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Mwanawe Rais Museveni, Muhoozi Kainerugaba atangaza nia ya kununua Manchester United

Muhoozi amesema kuwa Uganda sasa ina rasilimali za kutosha kununua moja ya timu kubwa za soka za Uingereza.

image
na Samuel Mainajournalist

Football24 February 2025 - 08:43

Muhtasari


  • “Uganda sasa ina fedha za kutosha kununua moja ya timu hizo za soka za Uingereza! Tununue ipi?" Muhoozi alisema.
  • Muhoozi alibainisha kuwa klabu atakayonunua italazimika kuvaa jezi zilizoandikwa ‘Visit Uganda’.

Gen Muhoozi Kainerugaba

Muhoozi Kainerugaba, mwanawe rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni, ameelezea nia yake ya kununua klabu ya soka ya Manchester United.

Akizungumza kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii  X siku ya Jumapili, mwanawe rais Museveni alisema kuwa Uganda sasa ina rasilimali za kutosha kununua moja ya timu kubwa za soka za Uingereza.

Ili kusisitiza hoja yake, aliwauliza Waganda wanataka anunue klabu gani.

“Uganda sasa ina fedha za kutosha kununua moja ya timu hizo za soka za Uingereza! Tununue ipi?" Muhoozi aliandika kwenye moja ya Tweets zake.

Katika tweet yake iliyofuata, alisema, "Manchester United inagharimu kiasi gani cha pesa", kuashiria kwamba ana nia ya kununua klabu inayoshabikiwa na wengi.

Muhoozi ambaye pia ni Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Uganda (UPDF) alibainisha kuwa klabu atakayonunua italazimika kuvaa jezi zilizoandikwa ‘Visit Uganda’.

"Waganda, nafasi ya mwisho. Arsenal, Manchester United, Chelsea… timu yoyote utakayochagua italazimika kuvaa chapa ya Visit Uganda,” alisema.

Kwa sasa, hakuna klabu ya soka ya Uingereza inayomilikiwa na Mwafrika.

Manchester United, ambayo Muhoozi ameonyesha nia ya kununua, bado inamilikiwa na familia ya Glazer, lakini mabadiliko makubwa yalifanyika mapema 2024 baada ya bilionea wa Uingereza, Sir Jim Ratcliffe, kununua asilimia 25 ya hisa za klabu kwa takriban pauni milioni 1.3.

Kupitia kampuni yake ya INEOS, Ratcliffe alipata udhibiti wa masuala ya kandanda ndani ya klabu, ikiwa ni pamoja na usimamizi wa usajili wa wachezaji, miundombinu, na maendeleo ya kikosi.

Kwa sasa, familia ya Glazer inamiliki asilimia kubwa ya hisa za klabu (takriban 69%), ikiwa ni pamoja na hisa zenye haki ya kupiga kura. Hata hivyo, Sir Jim Ratcliffe, licha ya kuwa na hisa chache, ana ushawishi mkubwa katika uendeshaji wa klabu. Sehemu nyingine ya hisa inamilikiwa na wanahisa wa umma kupitia soko la hisa la New York (NYSE), lakini hawana mamlaka makubwa katika maamuzi ya klabu.

Baada ya uwekezaji wa INEOS, kumekuwa na mabadiliko makubwa katika uongozi wa klabu. Moja ya hatua kuu zilizochukuliwa ni kumleta Omar Berrada kutoka Manchester City kama Afisa Mkuu Mtendaji mpya wa United. Hatua hii inaashiria mipango ya klabu kuboresha usimamizi wake wa masuala ya mpira wa miguu.

Aidha, Ratcliffe amesisitiza kuwa klabu inatarajia kufanya maboresho makubwa ya miundombinu, ikiwemo Uwanja wa Old Trafford na kituo cha mazoezi cha Carrington.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved