logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Sergio Aguero apoteza bet ya milioni 1.5 baada ya kuweka imani yake kwa Man City

Aguero alikuwa ameonyesha matumaini yake makubwa kwa klabu yake ya zamani kushinda dhidi ya Liverpool.

image
na Samuel Mainajournalist

Football24 February 2025 - 11:58

Muhtasari


  • Aguero alikuwa ameweka dola 5,000 (Sh647,250) kwa Man City kushinda ambapo angepata $11,300 (Sh 1.46m).
  • Hii ni mara ya pili imani ya Muargentina huyo kwa Man City inamletea shida katika kipindi cha mwezi  mmoja uliopita.

Sergio Aguero

Mshambulizi wa zamani wa klabu ya Manchester City na timu ya taifa ya Argentina Sergio Kun Aguero alipoteza dau lingine Jumapili kufuatia vijana wa Pep Guardiola kuchapwa na Liverpool.

Aguero alikuwa ameonyesha matumaini yake makubwa kwa klabu yake ya zamani kushinda katika mechi hiyo kubwa iliyochezwa katika uwanja wa Etihad kwa kuwekelea dau kubwa.

Muargentina huyo mwenye umri wa miaka 36 alikuwa ameweka dola 5,000 (Sh647,250) kwa Man City kushinda ambapo angepata $11,300 (Sh 1.46m) kama malipo.

Man City hata hivyo walipokea kichapo katika uwanja wao wa nyumbani huku The Reds wakiondoka na ushindi wa 0-2, kumaanisha dau la Aguero liliungua.

Hii ni mara ya pili imani ya Muargentina huyo kwa klabu yake ya zamani inamletea shida katika kipindi cha mwezi  mmoja uliopita.

Takriban wiki mbili zilizopita, Aguero alijikuta katika hali ya utata baada ya ahadi yake tata kabla ya mechi ya Ligi ya Mabingwa kati ya Manchester City na Real Madrid.

Kabla ya mchuano huo uliofanyika kwenye uga wa Etihad, Agüero alitoa kauli yenye utata akisema, "Ikiwa Real Madrid itashinda, nitakata tezi ndume zangu."

Maneno haya, ambayo yalionekana kama mzaha wa kuonesha imani yake kwa City, sasa yamegeuka mzigo mzito baada ya Real Madrid kuibuka na ushindi wa 2-3.

Katika mechi hiyo ya mchujo ya Ligi ya Mabingwa, Manchester City walijikuta wakizidiwa nguvu na Los Blancos, huku magoli ya Kylian Mbappe, Brahima Diaz na Jude Bellingham yakiwapa ushindi wenye thamani kubwa.

Hali hii ilisababisha mashabiki wa soka, hususan wale wa Real Madrid, kumbana Agüero kuhusu ahadi yake isiyo ya kawaida.

Baada ya kipenga cha mwisho kulia, mitandao ya kijamii ilifurika jumbe kutoka kwa mashabiki waliomkumbusha Agüero juu ya ahadi yake. Wengine walienda mbali zaidi na kuunda vibonzo vya kejeli, wakimuuliza lini anapanga kutimiza maneno yake.

Agüero, ambaye kwa sasa ni mchambuzi wa soka na mtangazaji wa mitandaoni, hakutoa tamko rasmi kuhusu ahadi hiyo, lakini amekuwa akichukulia mzaha shinikizo linaloendelea.

Hata hivyo, mashabiki wengi walielewa kuwa kauli yake ilikuwa tu njia ya kusisitiza uaminifu wake kwa Manchester City na hakuwa na nia ya kweli ya kutekeleza alichosema.


Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved