

Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola, ameonyesha matumaini makubwa kwa timu yake licha ya kupoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Liverpool katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza iliyochezwa Jumapili, Februari 23, 2025, kwenye uga wa Etihad.
Katika mahojiano baada ya mchezo, Guardiola alieleza kuwa kikosi chake kilicheza vizuri na kwamba anaamini kizazi kipya cha wachezaji wake kitakuwa msingi imara wa klabu hiyo kwa miaka ijayo.
"Isipokuwa Kevin De Bruyne na Nathan Aké, kikosi chetu kilikuwa na wachezaji vijana sana. Hili ni jambo la kutia moyo kwa mustakabali wa klabu," alisema Guardiola.
Licha ya kushindwa, Manchester City walionyesha mchezo mzuri, lakini Liverpool waliweza kuibuka na ushindi kupitia mabao ya Mohamed Salah na Dominik Szoboszlai.
Matokeo hayo yameifanya City kushindwa kupunguza pengo la alama dhidi ya viongozi wa ligi, Liverpool, na kuongeza ushindani mkali wa kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa msimu ujao.
Kwa kipigo hicho, Manchester City wamepata hasara kubwa katika mbio za kuwania nafasi nne za juu.
Hadi sasa, wapo nyuma kwa alama 20 dhidi ya Liverpool, huku klabu kama Aston Villa, Newcastle, na Nottingham Forest zikionekana kuwa wapinzani wakuu katika kinyang’anyiro cha nne bora.
"Tunapaswa kupambana zaidi kwa sababu ushindani ni mkali sana. Timu kadhaa zinataka nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa, na hatuna budi kufanya kazi kwa bidii ili kufanikisha hilo," aliongeza Guardiola.
Katika mechi hiyo, mashabiki wa Liverpool walikuwa wakimshambulia Guardiola kwa maneno wakimwambia kuwa ataondolewa kama kocha wa City.
Hata hivyo, kocha huyo wa Kihispania aliwajibu kwa ishara ya kuinua vidole sita, akimaanisha mataji sita ya EPL aliyoshinda na timu hiyo.
"Sikutarajia hilo kutoka kwa mashabiki wa Anfield. Tumekuwa na pambano kali kati yetu kwa miaka mingi. Sijali sana maneno yao, mimi naangazia maendeleo ya timu yangu," alisema Guardiola.
Guardiola pia alizungumzia hali ya mshambuliaji wake nyota, Erling Haaland, ambaye hakucheza dhidi ya Liverpool licha ya vipimo vya kitabibu kuonyesha hana jeraha lolote.
"Erling hakujihisi sawa kabla ya mchezo, lakini natarajia atakuwa fiti kwa mechi ijayo dhidi ya Tottenham Hotspur," alisema Guardiola.
Licha ya changamoto wanazokumbana nazo, Guardiola anasalia na
imani kuwa Manchester City itarejea kwenye kiwango bora na kupambana hadi
mwisho wa msimu kwa nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya.