
Kocha wa Liverpool, Arne Slot, amepewa marufuku ya mechi mbili baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu katika sare ya 2-2 dhidi ya Everton kwenye Uwanja wa Goodison Park mnamo Februari 12.
Slot alipokea adhabu hiyo baada ya kumfuata mwamuzi Michael Oliver uwanjani mara baada ya mechi kumalizika.
Hii inamaanisha hatakuwa kwenye benchi la ufundi wakati Liverpool itakapocheza dhidi ya Newcastle nyumbani Jumatano hii, pamoja na mechi dhidi ya Southampton mnamo Machi 8.
Hata hivyo, ataruhusiwa kuwa kwenye benchi la ufundi wakati Liverpool itakapokabiliana na Paris Saint-Germain kwenye hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mnamo Machi 5.
Mbali na marufuku hiyo, Slot pia amepewa faini ya pauni 70,000 na kamati huru ya Shirikisho la Soka la England (FA) baada ya kukubali mashtaka dhidi yake.
Kocha msaidizi wa Liverpool, Sipke Hulshoff, naye amefungiwa mechi mbili na kutozwa faini ya pauni 7,000. Aidha, klabu ya Liverpool imepigwa faini ya pauni 65,000 huku Everton wakitozwa pauni 50,000 kwa kushindwa kudhibiti wachezaji wao wakati wa mchezo huo.
Machafuko yalizuka baada ya James Tarkowski kufunga bao la kusawazisha katika dakika ya 98, hali iliyosababisha mashabiki wa Everton kuingia uwanjani kusherehekea. Liverpool walilalamikia bao hilo, wakidai Tarkowski alimsukuma beki wao, Ibrahima Konate, katika harakati za kulifunga.
Baada ya mchezo, Slot alionekana kubadilishana maneno na mmoja wa waamuzi wasaidizi kabla ya kumpa mkono mwamuzi Oliver, ambaye alimpatia kadi nyekundu papo hapo. Hulshoff naye alifukuzwa.
Kutokana na kadi nyekundu hiyo, Slot hakuruhusiwa kuzungumza na vyombo vya habari baada ya mechi. Hata hivyo, siku mbili baadaye katika mkutano na waandishi wa habari, alieleza kuwa "hisia zilimpata" kutokana na muda wa nyongeza uliochezwa kuwa mrefu zaidi ya ilivyotangazwa awali.
Katika mchuano huo mkali, wachezaji Abdoulaye Doucoure wa Everton na Curtis Jones wa Liverpool walionyeshwa kadi nyekundu baada ya filimbi ya mwisho kwa makosa ya kadi ya pili ya njano. Wote wawili walikosa mechi moja kutokana na adhabu hiyo.
Slot atarejea kwenye benchi la ufundi baada ya mapumziko ya mechi za kimataifa, wakati Liverpool itakapomenyana na Newcastle katika fainali ya Kombe la Carabao mnamo Machi 16.
Kwa sasa, Liverpool wanaongoza Ligi Kuu ya England kwa tofauti ya alama 11 na wanatarajiwa kumenyana tena na Everton katika uwanja wa Anfield mnamo Aprili 2.
Slot pia amewahi kuhudumu marufuku ya kukosa mechi wakati wa robo fainali ya Kombe la EFL dhidi ya Southampton mnamo Desemba baada ya kuonyeshwa kadi tatu za njano.