
Katika usiku wa tarehe 11 Machi 2025, mashabiki wa soka ulimwenguni kote walishuhudia matukio mengi na mechi za kusisimua katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Hata hivyo, tukio lililovuta hisia za wengi ni mshambuliaji nyota wa Liverpool, Mohamed Salah, ambaye alionekana akitokwa na machozi baada ya timu yake kuondolewa kwenye mashindano hayo na Paris Saint-Germain (PSG).
Mchuano huo uliochezwa katika uwanja wa Anfield ulianza kwa kasi, huku timu zote zikionyesha nia ya kusonga mbele, kabla ya PSG kufunga katika dakika za mapema. .
Licha ya juhudi zao, Liverpool walishindwa kupata bao katika muda wa kawaida na ule wa nyongeza baada ya PSG kufanikiwa kupata bao muhimu kupitia kwa mshambulizi Ousmane Dembele katika dakika ya 12, na kufanya matokeo kuwa 1-0 katika mchezo huo, hivyo kusawazisha jumla ya mabao kuwa 1-1 baada ya Liverpool kushinda 1-0 katika mchezo wa kwanza.
Hatma ya mchezo iliamuliwa kupitia mikwaju ya penalti, ambapo PSG walionyesha ubora mkubwa.
Kipa wao, Gianluigi Donnarumma, aliokoa penalti za Darwin Núñez na Curtis Jones, huku Mohamed Salah akiwa mchezaji pekee wa Liverpool aliyefunga penalti yake.
Kwa upande wa PSG, wachezaji wao walikuwa na utulivu na kuhakikisha wanapata ushindi huo muhimu. Vitinha, Goncalo Ramos, Ousmane Dembele, na Desire Doue wote waliweza kufunga mikwaju ya penalty na kufanikisha ushindi huo ambao ulimaanisha kubanduliwa kwa Liverpool nje ya mashindano hayo.
Hisia za Salah zilionekana wazi baada ya mchezo, ambapo alionekana akikalia magoti akiwa ameshika uso wake, kisha kusimama huku machozi yakimtoka. Hii inaonyesha jinsi mchezaji huyo anavyothamini michuano hii na jinsi alivyoguswa na matokeo hayo ya kuvunja moyo.
Katika michezo mingine ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyochezwa tarehe 11 Machi 2025, Bayer Leverkusen walipoteza nyumbani kwa mabao 0-2 dhidi ya Bayern Munich, hivyo kubanduliwa nje ya Ligi ya Mabingwa pia.
Inter walipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Feyenoord. Barcelona nao wakashinda 3-1 dhidi ya Benfica na kujihakikishia nafasi kati robo fainali ya Ligi ya Mabingwa.
Leo, tarehe 12 Machi 2025, mashabiki wa soka wanatarajia kuona mechi nyingine za kusisimua katika michuano hii.
Ratiba inaonyesha kuwa kutakuwa na michezo kadhaa muhimu huku
Arsenal ikimenyana na PSV ugani Emirates, Lille wakiwakaribisha Borrusia
Dortmund, Club Brugge KV watakuwa wageni wa Aston Villa na Atletico Madrid
watachuana na Real Madrid ugani Metropolitano.