EURO 2020

Mkwaju hafifu wa Mbappe waua ndoto za mabingwa wa kombe la dunia; Uhispania, Uswisi zapenya robo fainali

Jumla ya mabao 13 na penalti 9 zilifungwa kwenye mechi hizo mbili zilizopelekea kubanduliwa kwa timu mbili tajika

Muhtasari

•Wengi walitarajia mabingwa wa Kombe la dunia mwaka wa 2018, Ufaransa kupenya na kuhitimu kuingia robo fainali ila ndoto za mabingwa hao wa kombe la EURO mara mbili zilikatizwa kwenye mikwaju ya penalti.

•Mshambulizi wa Juventus, Alvaro Moratana Mikel Oyarzabal wa Real Sociedad walifungia Uhispania kwenye dakika za ziada na kuendeleza ndoto zake za kupata taji la nne la EURO.

Kyllian Mbappe baada ya kupoteza mechi dhidi ya Uswisi
Kyllian Mbappe baada ya kupoteza mechi dhidi ya Uswisi
Image: Instagram

Usiku wa Jumatatu ulishuhudia mechi mbili za kusisimua zaidi kwenye michuano inayoendelea ya EURO 2020.

Jumla ya mabao 13 na penalti 9 zilifungwa kwenye mechi hizo mbili zilizopelekea kubanduliwa kwa timu mbili tajika.

Mechi iliyoacha wengi vinywa wazi ni kati ya Ufaransa na Uswisi ambayo ilichezewa ugani Arena Nationala jijini Bucharest, Romania.

Wengi walitarajia mabingwa wa Kombe la dunia mwaka wa 2018, Ufaransa kupenya na kuhitimu kuingia robo fainali ila ndoto za mabingwa hao wa kombe la EURO mara mbili zilikatizwa kwenye mikwaju ya penalti.

Mechi hiyo ilichezwa hadi kufikia kupigwa kwa penalti baada ya kutoka sare ya 3-3 katika dakika 90 za kawaida.

Haris Seferovic alianza kufungia timu ya Uswisi katika dakika ya 15 kabla ya mshambulizi matata wa klabu ya Real Madrid kusawazishia Ufaransa katika dakika ya 57 na kuwapa uongozi dakika mbili baadae kwa kufunga bao la pili.

Kiungo wa Manchester United, Paul Pogba aliongeza matumaini ya Ufaransa kutwaa ushindi kwa kufungia timu hiyo bao la tatu katika dakika ya 75. 

Hata hivyo, simba aliyekuwa amelala aliamka katika dakika za mwisho mwisho huku Seferovic akifungia Uswisi bao la pili dakika 9 tu kabla ya 90 za kawaida kutimia naye Mario Gavranovic akasawazisha mechi katika dakika ya lala salam.

Dakika 30 za ziada hazikushuhudia bao lolote na hapo ikabidi mechi kuamuliwa na penalti.

Uswisi ilifunga penalti zake tano zote kupitia Mario Gavranovic, Fabian Schar, Manuel Akanji, Ruben Vargas na Admir Mehmedi.

Mkwaju wa Kylian Mbappe ulishikwa na mlinda lango Yann Sommer wa Uswisi na kusaidia wapinzani kushinda licha ya Paul Pogba, Olivier Giroud, Marcus Thuram na Presnel Kimpembe kufunga mikwaju yao hapo awali.

Kwenye mechi iliyokuwa imechezwa hapo awali, Uhispania ilibandua Croatia kutoka kwenye michuano ya EURO kwenye dakika za ziada.

Mechi hiyo iliishia sare ya 2-2 kwenye dakika 90 za kawaida na ikabidi iende hadi dakika za ziada.

Bao la kujifunga la kiungo wa Barcelona lilipatia Croatia uongozi kabla ya Pablo Sarabia , Ceasar Azpilicueta na Ferran Torres  kufufua ndoto za Uhispania katika dakika ya 38 , 57 na 77.

Hata hivyo, Croatia waliamka dakika za mwisho mwisho huku Mislav Orsic na Mario Pasalic wakifunga katika dakika ya 85 na 92 mtawalia.

Mshambulizi wa Juventus, Alvaro Moratana Mikel Oyarzabal wa Real Sociedad walifungia Uhispania kwenye dakika za ziada na kuendeleza ndoto zake za kupata taji la nne la EURO.