MATOKEO YA EURO 2020

EURO 2020: Mataifa manne yahitimu kuingia robo fainali, Mabingwa wabanduliwa nje

Ubelgiji itamenyana na Italia kwenye mkondo wa robo fainali huku Ucheki ikikabiliana na Denmark.

Muhtasari

•Timu mbili ambazo ziliwashangaza wengi kwa kuondolewa kwenye michuano hiyo ni washindi wa kombe la EURO 2016, Ureno na mabingwa wa Uholanzi.

•Mechi kati ya Croatia na Uhispania pamoja na mechi kati ya Ufaransa na Uswizi zinatarajiwa kuchezwa siku ya Jumatatu huku Uingereza dhidi ya Ujerumani na mechi kati ya Uswidi na Ukraine zikichezwa Jumanne kubaini nani atakayehitimu kuingia robo fainali.

Christiano Ronaldo wa Ureno baada ya kupoteza mechi dhidi ya Ubelgiji
Christiano Ronaldo wa Ureno baada ya kupoteza mechi dhidi ya Ubelgiji
Image: Hisani

Drama inaendelea kushuhudiwa kwenye michuano ya EURO 2020 ambayo inaelekea kuingia kwenye mkono wa robo fainali.

Mnamo wikendi, mataifa nane yalicheza huku manne yakibanduliwa nje tayari na manne yakihitimu kuingia robo fainali.

Timu mbili ambazo ziliwashangaza wengi kwa kuondolewa kwenye michuano hiyo ni washindi wa kombe la EURO 2016, Ureno na mabingwa wa Uholanzi.

Ureno hawataweza kuhifadhi kombe hilo baada ya kupoteza mechi dhidi ya Ubelgiji usiku wa Jumapili.

Timu hiyo ambayo inaongozwa na mshambulizi matata, Christiano Ronaldo ilipigwa bao moja kwa sufuri kwenye mechi ya kusisimua.  Bao la Ubelgiji lilifungwa na kiungo wa Borussia Dortmund,Thorgan Hazard katika dakika ya 42.

Awali siku hiyo, timu ya Uholanzi ilichapwa mabao mawili bila jawabu na timu ya Ucheki. Mabao ya Tomas Holes na Patrik Schick yaliua ndoto za taifa hilo ambalo lilicheza kwenye fainali ya Kombe la dunia mwaka wa 2010.

Austria na Wales zilikuwa zimetangulia kubanduliwa nje kwenye kombe hilo siku ya Jumamosi.

Denmark ilipatia wenyeji Wales kichapo kikubwa cha mabao manne kwa sufuri kufuatia mabao mawili ya Kasper Dolberg wa klabu ya Nice, moja la Joakim Maehle wa Atlanta na lingine la mshambulizi wa Barcelona Martin Braithwaite.

Kiungo wa Wales na klabu ya Liverpool, Harry Wilson alipewa kadi nyekundu baada ya kuangusha mchezaji wa Denmark kwenye dakika za mwisho.

Italia ilifaulu kuhitimu kuingia robo fainali baada ya kucharaza Austria mabao mawili kwa moja kwenye mechi ambayo ilichezwa hadi dakika za ziada.

Mabao yote matatu yalifungwa katika dakika za maongezi baada ya mechi hiyo kuisha sare tasa katika dakika 90 za kawaida.

Mshambulizi wa Juventus Federico Chiesa alianza kufungia Italia kwenye dakika ya 95 kabla ya Matteo Pessina wa Atlanta kufungia Italia la pili dakika kumi baadae. Sasa Kalajdzic alifungia Austria bao la kipekee katika dakika ya 114.

Mechi kati ya Croatia na Uhispania pamoja na mechi kati ya Ufaransa na Uswizi zinatarajiwa kuchezwa siku ya Jumatatu huku Uingereza dhidi ya Ujerumani na mechi kati ya Uswidi na Ukraine zikichezwa Jumanne kubaini nani atakayehitimu kuingia robo fainali.

Ubelgiji itamenyana na Italia kwenye mkondo wa robo fainali huku Ucheki ikikabiliana na Denmark.