Klabu ya soka ya Manchester United imethibitisha kuondoka kwa winga Jadon Sancho.
Katika taarifa ya Alhamisi mchana, klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Uingereza ilithibitisha kwamba staa huyo wa soka mwenye umri wa miaka 23 amejiunga tena na klabu yake ya zamani, Borrusia Dortmund.
Uhamisho wa Sancho hata hivyo sio wa kudumu kwani amejiunga tena na timu hiyo ya Ujerumani kwa mkopo hadi mwisho wa msimu wa EPL 2023/24.
"Sancho sasa atarejea Ujerumani kwa muda huku Borussia Dortmund wakijiandaa kuanza tena kampeni yao ya Bundesliga baada ya mapumziko ya msimu wa baridi. Mchezaji huyo wa kimataifa wa Uingereza aliyecheza mechi za kimataifa 23 anaondoka na tunawatakia heri katika kipindi kilichosalia cha msimu huu,” Man United ilisema katika taarifa iliyotumwa kwenye tovuti yake rasmi.
Borrusia Dortmund pia ilithibitisha kurejea kwa winga huyo mwenye umri wa miaka 24 na kufichua kwamba atasalia katika klabu hiyo hadi Juni 30, 2024.
Wakati akitangaza kurejea kwake, mchezaji huyo alisema anajivunia sana kujiunga tena na klabu hiyo ya Ujerumani na kusema kwamba ana hamu ya kuicheza tena.
“Halo mashabiki wa BVB. Hapa ni kwa Jadon. Nataka tu kusema heri ya mwaka mpya. Nimefurahi sana kurejea na siwezi kusubiri kuanza. Ona uone na utunze,” Sancho alisema kwenye video aliyorekodi.