
Klabu ya Manchester United inayoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza imeanza kutekeleza mpango wa kupunguza gharama kwa kiasi kikubwa.
Hatua hizi znahusisha kufutwa kwa hadi wafanyakazi 200 na kuondolewa kwa milo ya bure kwa wafanyakazi waliopo.
Hatua hizi zinakuja wakati klabu hiyo ikiendelea kukabiliana na changamoto za kifedha baada ya kurekodi hasara kwa miaka mitano mfululizo.
Kwa mujibu wa taarifa, mipango hii inasimamiwa na mmiliki mwenza mpya wa klabu, Sir Jim Ratcliffe, na kampuni yake ya INEOS, ambayo ilinunua asilimia 27.7 ya hisa za Manchester United.
Lengo kuu la hatua hizi ni kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kuhakikisha klabu inarejea katika hali thabiti ya kifedha.
Mojawapo ya hatua kali zaidi ni kupunguzwa kwa wafanyakazi, ambapo inakadiriwa kuwa takriban wafanyakazi 200 watapoteza kazi zao.
Idara zitakazoathirika zaidi bado hazijawekwa wazi, lakini vyanzo vya ndani vya klabu vinasema kuwa zoezi hili litalenga hasa wafanyakazi wa ofisi na wale wasiohusiana moja kwa moja na timu ya kwanza.
Uongozi wa Manchester United unaamini kuwa idadi ya wafanyakazi ni kubwa mno kulinganisha na mahitaji halisi ya klabu, hasa kwa kuzingatia mazingira ya sasa ya kifedha.
Hatua nyingine iliyowashangaza wengi ni kufutwa kwa huduma ya chakula cha bure kwa wafanyakazi wa klabu katika viwanja vya Old Trafford na Carrington.
Kabla ya mabadiliko haya, wafanyakazi walikuwa wakipata milo kamili bila malipo, lakini sasa watapewa tu supu, mkate, na matunda.
Uamuzi huu unalenga kupunguza gharama ya chakula cha wafanyakazi kwa zaidi ya pauni milioni moja kwa mwaka, huku klabu ikitafuta njia za kupunguza matumizi katika kila sekta.
Hatua hizi zinachukuliwa wakati Manchester United ikiendelea kupitia kipindi kigumu ndani na nje ya uwanja.
Timu hiyo haijapata mafanikio makubwa tangu kuondoka kwa Sir Alex Ferguson mwaka 2013, na mashabiki wengi wana matumaini kwamba ujio wa Sir Jim Ratcliffe utasaidia kuleta mabadiliko chanya.
Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa soka na mashabiki wameeleza wasiwasi wao kuhusu athari za hatua hizi, hasa kwa wafanyakazi wa klabu waliokuwa wakiitegemea kwa riziki yao.
Kwa sasa, bado haijafahamika iwapo hatua hizi zitasaidia kuimarisha hali ya kifedha ya klabu kwa muda mrefu, lakini ni wazi kuwa uongozi wa Manchester United umeazimia kupunguza matumizi kwa gharama yoyote ile.