
Klabu ya FC Barcelona imepatwa na msiba mzito baada ya kifo cha ghafla cha daktari wao wa timu ya kwanza, Carles Miñarro García, mwenye umri wa miaka 50.
Tukio hilo la kuhuzunisha lilitokea muda mfupi kabla ya mechi yao ya La Liga dhidi ya Osasuna, iliyokuwa imepangwa kuchezwa Jumamosi katika Uwanja wa Estadi Olímpic Lluís Companys.
Miñarro García alijiunga na timu ya matibabu ya FC Barcelona msimu uliopita na alikuwa akiheshimiwa sana na wachezaji pamoja na wafanyakazi wenzake.
Kifo chake kimeacha pengo kubwa ndani ya klabu, na kusababisha maombolezo makubwa miongoni mwa wachezaji, viongozi, na mashabiki.
Kutokana na msiba huu, uongozi wa FC Barcelona, kwa kushirikiana na Osasuna na maafisa wa La Liga, waliamua kuahirisha mechi hiyo.
Katika taarifa yao rasmi, klabu hiyo ilieleza huzuni yao kubwa kwa kuondokewa na mtaalamu huyo wa tiba ya michezo.
"FC Barcelona inasikitika kutangaza kifo cha daktari wa timu ya kwanza, Carles Miñarro García, jioni ya leo. Kutokana na hili, mchezo kati ya FC Barcelona na CA Osasuna umeahirishwa hadi tarehe nyingine.
Bodi ya Wakurugenzi ya FC Barcelona na wafanyakazi wote tunatoa rambirambi zetu za dhati kwa familia na marafiki zake katika kipindi hiki kigumu," taarifa ilisomeka.
Baada ya mashauriano kati ya pande husika, mechi ya Barcelona dhidi ya Osasuna iliakhirishwa rasmi. Hadi sasa, La Liga bado haijatangaza tarehe mpya ya mchezo huo.
Kwa sasa, FC Barcelona inajikita katika maandalizi ya mechi yao ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Benfica, inayotarajiwa kufanyika Jumanne ijayo.