logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Mudavadi alaani vikali mashambulizi dhidi ya Salasya katika Uwanja wa Nyayo

Mudavadi alilaani vikali vitendo vya vurugu na kusisitiza haja ya umoja miongoni mwa Wakenya ili kuleta maendeleo.

image
na Samuel Mainajournalist

Football24 March 2025 - 08:00

Muhtasari


  • Mudavadi, amelaani vikali mashambulizi dhidi ya Mbunge wa Mumias Mashariki, Peter Salasya, wakati wa mechi ya Harambee Stars.
  • Mudavadi alitoa wito kwa Wakenya kukumbatia mazungumzo na kuheshimu mitazamo tofauti ya kisiasa.

Musalia Mudavadi amelaani mashambulizi dhidi ya mbunge Peter Salasya

Mkuu wa Baraza la Mawaziri, Musalia Mudavadi, amelaani vikali mashambulizi dhidi ya Mbunge wa Mumias Mashariki, Peter Salasya, wakati wa mechi ya Harambee Stars dhidi ya Gabon siku ya Jumapili, Machi 23.

Salasya alikuwa amefika katika Uwanja wa Nyayo kushuhudia mechi hiyo muhimu ya kufuzu Kombe la Dunia, lakini hakupata fursa ya kuitazama. Kabla ya mchuano huo kuanza, alishambuliwa na kundi la vijana waliomfurusha kutoka uwanjani kwa madai ya kumkosea heshima kiongozi wa chama cha ODM, Raila Amollo Odinga. Matokeo yake, alilazimika kutazama mechi hiyo kupitia runinga yake.

Kupitia ukurasa wake wa X Jumapili jioni, Mudavadi ambaye pia alikuwepo uwanjani, alielezea tukio hilo kama la kusikitisha. Alitoa wito kwa Wakenya kukumbatia mazungumzo na kuheshimu mitazamo tofauti ya kisiasa.

"Kutovumiliana kisiasa kunahujumu misingi ya demokrasia yetu, ambayo inategemea uwezo wa kushiriki mijadala yenye mitazamo tofauti. Hatutakubaliana daima, na hilo ni sawa. Lakini heshima, mazungumzo na umoja ni mambo yasiyopaswa kupuuzwa. Heshima inapaswa kutolewa, lakini pia inapaswa kupatikana kwa matendo," alisema Mudavadi.

Waziri Mkuu huyo alilaani vikali vitendo vya vurugu na kusisitiza haja ya umoja miongoni mwa Wakenya ili kuleta maendeleo.

"Ndugu zangu Wakenya, hakuna mtu mwingine atakayeijenga nchi hii kwa ajili yetu. Tukiruhusu mgawanyiko kushinda, tunahatarisha kudhoofisha kila kitu tunachotarajia kujenga. Nyumba iliyogawanyika haiwezi kusimama. Tuchague busara badala ya fujo, na ukomavu badala ya makelele. Mustakabali wa Kenya unategemea maamuzi yetu," aliongeza.

Katika video zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii Jumapili, Salasya, ambaye alikuwa amevalia jezi ya AFC Leopards, alionekana akishambuliwa na kundi la vijana waliomlazimisha kuelekea kwenye lango la kutoka uwanjani.

Baadhi yao walionekana wakimrushia vitu huku wachache wakijaribu kumlinda dhidi ya mashambulizi hayo.

Katika video nyingine, polisi walionekana wakiingilia kati na kumwondoa Salasya kutoka kwa kundi hilo, huku umati ukimfuata na baadhi yao wakisikika wakisema, "Lazima aheshimu Raila."

Baada ya kisa hicho, Salasya alitulia na kupitia ukurasa wake wa X akaandika kwa kifupi neno “imeeleweka”.

Katika chapisho lingine, mbunge huyo alisema kuwa licha ya kuwa na chaguo tofauti, aliamua kuchagua amani na ndiyo sababu hakujibu mashambulizi hayo.

"Sikutaka kuwa na damu mikononi mwangu. Ni sawa, nilikuwa na chaguzi lakini nilichagua amani," alisema Salasya kupitia X.

Hata hivyo, alionya kuwa iwapo jambo kama hilo litajaribiwa tena, hatakuwa mpole kama alivyokuwa safari hii.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved