Liverpool imefanikiwa kumhifadhi mshambuliaji wao nyota, Mohamed Salah, baada ya kusaini mkataba mpya wa miaka miwili utakaomuweka Anfield hadi mwaka 2027.
Mkataba wa awali wa mchezaji huyo wa miaka 32 ulikuwa unakamilika mwishoni mwa msimu huu, huku kukiwa na uvumi mkubwa kuhusu uwezekano wa kuhamia Saudi Arabia.
Kauli zake za awali na tetesi zilizomhusisha na vilabu vya Mashariki ya Kati zilionyesha hali ya kutokuwa na uhakika. Lakini sasa, Salah ameweka wazi kuwa bado ana nia ya kuendelea kuitumikia Liverpool.
“Nina furaha sana,” alisema Salah baada ya kusaini mkataba mpya.
“Tuna kikosi dhabiti na tunaamini tunaweza kushinda mataji zaidi. Nimekuwa hapa kwa miaka minane, natumai nitafikisha kumi,” aliongeza.
Tangu atue kutoka AS Roma mwaka 2017, Salah ameifungia Liverpool mabao 243 na kutoa pasi 109 za mabao katika mechi 394, rekodi inayoonyesha mchango wake mkubwa.
Katika msimu huu pekee, amefunga mabao 32 katika mashindano yote, wakiwemo 27 ya Ligi Kuu ya England, huku Liverpool wakisalia kileleni mwa msimamo wa ligi wakiwa na pointi 11 mbele ya Arsenal, mechi saba zikiwa zimebaki.
Nyota huyo wa Misri ameisaidia Liverpool kutwaa mataji ya Ligi Kuu ya England, Ligi ya Mabingwa Ulaya, FA Cup, League Cup, na Kombe la Dunia la Vilabu la FIFA.
Salah alikuwa mmoja wa wachezaji watatu wakongwe waliokuwa wakielekea kumaliza mikataba yao, sambamba na Virgil van Dijk na Trent Alexander-Arnold. Van Dijk amesema mazungumzo yanaendelea vyema, huku Alexander-Arnold akiendelea kuhusishwa na Real Madrid.
Mkataba wake wa awali ulimfanya kuwa mchezaji anayelipwa zaidi katika historia ya Liverpool, akilipwa zaidi ya pauni 350,000 kwa wiki. Inaelezwa kuwa mkataba mpya hauhusishi kupunguzwa kwa mshahara.