
Msimu wa Leicester City umeisha kwa masikitiko makubwa, huku nahodha wao Jamie Vardy akielezea kampeni ya mwaka huu kama "ya kuhuzunisha" na "aibu kubwa" baada ya kushushwa daraja kutoka Ligi Kuu ya Uingereza.
Leicester walithibitishwa kurejea Championship mara moja kufuatia kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Liverpool siku ya Jumapili. Hii ni mara ya pili ndani ya misimu mitatu klabu hiyo kushushwa daraja—ikiwa ni anguko kubwa kwa timu iliyowahi kushangaza ulimwengu kwa ubingwa wa kihistoria.
“Hakuna maneno ya kuelezea kwa ukamilifu hasira na huzuni ninayohisi kuhusu jinsi msimu huu umeenda. Hatuna visingizio,” Vardy aliandika kupitia mitandao ya kijamii akiwa na majonzi makubwa.
“Aidha, kwa kuwa nimekuwa hapa kwa muda mrefu, nimepitia mafanikio makubwa na nyakati za fahari. Lakini msimu huu umekuwa wa huzuni tupu—na binafsi, ni aibu ya kiwango cha juu. Inauma sana, na najua mashabiki wetu nao wanaumia,” aliandika.
“Kwa mashabiki wetu: Samahani. Samahani hatukuweza kuonyesha makali tuliyotarajiwa.”
Vardy alikuwa sehemu muhimu ya kikosi kilichotwaa ubingwa wa Ligi Kuu mwaka 2015/16, kabla ya kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa msimu uliofuata. Pia alishinda Kombe la FA na Ngao ya Jamii mwaka 2021, akichangia katika enzi ya mafanikio ya kihistoria ya klabu hiyo.
Hata hivyo, msimu huu umekuwa tofauti kabisa. Leicester wapo nafasi ya 19 kwenye jedwali, wakiwa na alama 18 pekee kutokana na mechi 33. Uteuzi wa Ruud van Nistelrooy kuwa kocha mwezi Novemba haukuleta mabadiliko yoyote, na sasa Leicester hawawezi hata kufikia alama 34 walizopata waliposhushwa daraja mara ya mwisho.
Tangu alipojiunga na klabu hiyo kutoka Fleetwood Town mwaka 2012, Vardy ameichezea Leicester mechi 496. Alifunga mabao 18 msimu uliopita walipotwaa ubingwa wa Championship, lakini msimu huu amefunga mabao saba pekee katika ligi.