Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang'i ametangaza Jumatatu Agosti 29 kuwa likizo ya umma katika maeneo manane ambapo uchaguzi mkuu uliahirishwa na tume ya IEBC kutokana na mkanganyiko wa karatasi za kupiga kura.
Maeneo hayo ni pamoja na; Kaunti za Mombasa na Kakamega. Maeneo mengine yaliyokabidhiwa likizo hiyo ni; Majimbo ya Kitui Rural, Kacheliba, Pokot na Rongai.
Wadi ya Kwa Njenga iliyopo Embakasi jijini Nairobi na Nyaki Magharibi iliyoko Imenti pia zitakuwa na likizo hiyo fupi ili kupisha wakaazi kutekeleza wajibu wao wa kidemokrasia.
Kulingana na taarifa ya Waziri Matiang’i, amewataka waajiri kote nchini kuwaachilia waajiriwa ambao ni wapiga kura katika maoneo hayo ambayo yalitangazwa na kuchapishwa kwenye gazeti la serikali ili kuenda kupiga kura.
"Waajiri kote nchini wanaombwa kuwaachilia wafanyikazi wao ambao wamejiandikisha kupiga kura katika maeneo yaliyoorodheshwa ya uchaguzi ili kuwawezesha kupiga kura," alisema Matiang'i.
Uchaguzi wa ugavana wa Mombasa na Kakamega uliahirishwa kwa mara ya kwanza mnamo Agosti 9 baada ya tume hiyo kugundua baadhi ya makosa kwenye karatasi za kupigia kura.
Uchaguzi huo ulipangwa kufanyika Agosti 23, lakini uliahirishwa tena.
Wakati wa mkutano na wagombeaji hao jijini Nairobi, mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alithibitisha Jumatatu, Agosti 29, kuwa tarehe mpya ya uchaguzi unaosubiriwa.
Mjini Mombasa, ODM imemkabili Mbunge wa Mvita anayeondoka Abdulswamad Nassir kuchuana na Hassan Omar wa UDA - ambaye alihudumu kama Seneta wa kwanza wa Mombasa hadi 2017.
Huko Kakamega, aliyekuwa mkuu wa Ketraco Fernandes Barasa atamenyana na seneta anayeondoka Cleophas Malala wa UDA katika azma ya kumrithi gavana Oparanya anayeondoka baada ya kuhudumu kama gavana kwa miaka 10.