Utangazaji wa matokeo ya kinyang'anyiro cha ugavana katika kaunti ya Narok uliahirishwa kutoka leo jioni hadi tarehe isiyojulikana kutokana na sababu za kiusalama.
Kulikuwa na mvutano katika kituo cha kujumlishia kura cha kaunti cha Maasai Mara University baada ya wafuasi wa wagombea wawili kutishia kuvamia.
Vyanzo vya habari katika kituo hicho vilisema kuwa moja ya sababu zilizowafanya kusitisha matangazo ni kwa sababu matokeo kutoka eneo bunge la Kilgoris yalichelewa kufika.
Mchana maafisa wa polisi walilazimika kuwarushia vitoa machozi vijana hao waliozua ghasia wakidai haki katika mchakato wa uchaguzi.
Usalama katika kituo cha kujumlisha kura umeimarishwa kwa kutumwa kwa maafisa wa GSU.
Mgombea wa ODM Moitalel ole Kenta alizuru kituo hicho na kuwaambia maafisa wa IEBC kutotangaza mshindi kwa madai kuwa zoezi hilo lilikumbwa na wizi na utovu wa nidhamu.
Katika mkutano wa faragha na viongozi, ambapo vyombo vya habari havikuruhusiwa kuingia, Kenta alitoa wito wa kuhesabiwa upya kwa kura.
"Watu sita wamekamatwa na madai ya wizi na wote wamekubali kwamba walihongwa ili kuendesha uchaguzi," Kenta alisema.
Mgombea ugavana wa UDA Patrick ole Ntutu, mbunge wa Emurua Dikirr Johana Ngeno na wafuasi wao tayari walikuwa wamefika kituoni hapo saa sita mchana tayari kupokea cheti cha mshindi.
Ntutu alisema ameshinda uchaguzi huo na atapewa cheti hicho Jumapili asubuhi.
"Tumeshinda uchaguzi huu na kesho asubuhi, tutapata cheti na kuanza sherehe za ushindi wetu," Ntutu alisema.
Wakati huo huo, mwenyekiti wa chama cha wafanyabiashara wa Narok David Mpatiany amewaonya waandishi dhidi ya kuchapisha habari za uongo kuhusu uchaguzi.
Mpatiany alisema vyombo vya habari vinapaswa kulinda uaminifu na usahihi wakati wa matangazo ya uchaguzi.
Alitaja habari potofu kwa mvutano wa sasa unaoshuhudiwa katika kinyang'anyiro cha ugavana wa Narok.
“Baadhi ya wanahabari walianza kuripoti kuwa mgombeaji fulani alishinda hata kabla ya IEBC kutoa matangazo rasmi. Vyombo vya habari lazima viwe na maadili katika kuandika habari za uchaguzi,” Mpatiany alisema.
Mwenyekiti huyo aliwataka wafanyabiashara kutokuwa na hofu na kuendelea na biashara zao akisema serikali imeimarisha ulinzi.
“Nawaomba muwe watulivu tunaposubiri matokeo ya mwisho msitishwe na mtu yeyote. Serikali imetuhakikishia kuwa watatoa usalama kwa hivyo hakuna cha kuhofia,” akasema.