logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Mtangazaji Gidi awasherehekea wanawake maalum katika maisha yake kwa njia ya kipekee

Gidi alisherehekea siku ya wanawake na mama yake mpendwa na dada zake wanne.

image
na Radio Jambo

Habari09 March 2023 - 05:09

Muhtasari


•Gidi alibainisha kuwa kitendo hicho ni zawadi bora zaidi ambayo angeweza kuwapa wanawake hao maalum katika maisha yake mnamo siku ya kuwasherehekea wanawake duniani.

•Gidi alisema siku ya wanawake ni maalum ya kutambua haki za wanawake na kubainisha kuwa yeye na  Ghost wanatambua mchango wa wanawake.

awaandalia mama na dada zake chakula cha jioni nyumbani kwake

Mnamo Jumatano, Machi 8, ulimwengu wote uliadhimisha siku ya wanawake duniani. Watu kote ulimwenguni walisherehekea siku hiyo maalum kwa njia zao za kipekee, ingawa wengine hata hivyo hata hawakuitambua.

Mtangazaji wetu wa kipindi cha asubuhi, Joseph Ogidi almaarufu Gidi alisherehekea siku hiyo pamoja na mama yake mpendwa na dada zake wanne.

Gidi aliwakaribisha wanafamilia hao watano nyumbani kwake na kuwaandalia chakula kizuri cha jioni ambacho walikula pamoja kama familia. Alibainisha kuwa kitendo hicho ni zawadi bora zaidi ambayo angeweza kuwapa wanawake hao maalum katika maisha yake mnamo siku ya kuwasherehekea wanawake duniani.

"Zawadi bora zaidi ambayo ningeweza kutoa ni kuwapikia mama na dada zangu katika siku ya kimataifa ya wanawake. Chakula cha jioni cha nyumbani," alisema kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Instagram.

Mtangazaji huyo mahiri aliambatanisha ujumbe wake na picha nzuri yake akiwa amekaa mezani na wanafamilia hao wake. Mezani, wanafamilia hao walikuwa na ugali, sukuma na nyama kama chakula chao cha jioni.

Awali siku hiyo, mwimbaji huyo wa zamani aliwasherehekea wanawake wote na kuwatakia heri ya siku ya wanawake duniani.

"Mimi na mwenzangu bwana Jacob 'Ghost' Mulee tungependa kuchukua fursa hii kuwatakia siku njema wanawake wote na kuwakumbusha kuwa wanawake ni watu muhimu sana katika maisha yetu kama jamii kwa sababu wanaume, wanawake, watoto, kila mmoja lazima amepitia kwa mwanamke," Gidi alisema.

Mtangazaji huyo mzoefu alisema siku ya wanawake duniani ni siku maalum ya kutambua haki za wanawake na kubainisha kuwa yeye na mtangazaji mwenzake, Ghost Mulee wanatambua sana mchango wa wanawake maishani.

"Mwanamke ni mtu ambaye ana haki kama mtu mwingine. Kuna mambo mengi ambayo wameweza kutekeleza katika maisha yetu. Tunajua kina mama zetu, mabibi zetu hata dada zetu wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba maisha yetu ni mema kuanza kutulea na mambo kama hayo. Tunawatambua sana wanawake kote duniani."

Ghost kwa upande wake alipongeza maendeleo ya nchi katika kuwashirikisha wanawake katika utawala. Aidha, aliwapongeza wanawake wote duniani kwa mchango wao mkubwa katika maendeleo ya dunia.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved