Kipindi cha mazungumzo na burudani ya kipekee cha Rombosa
Extra, kinachorushwa hewani na Radio Jambo kila Jumamosi kuanzia saa moja jioni
hadi saa nne usiku sasa kitawashirikisha mwandishi wa habari za michezo Tony
Mballa na DJ Uche Adi Rasta.
Watangazaji hao wawili wanatarajiwa kuwavutia wasikilizaji kwa
mijadala mikali kuhusu Ligi Kuu ya Uingereza, La Liga ya Uhispania, Bundesliga
ya Ujerumani na Ligue One ya Ufaransa, kipindi hicho kinapoingia wiki yake ya nne
Jumamosi ijayo.
Isitoshe, wawili hao wataangazia habari za soka za kitaifa,
ikiwa ni pamoja na kudadisi matokeo ya Ligi Kuu ya Kenya na ligi ya daraja la
pili ya Ligi Kuu ya Kitaifa.
Mballa, ambaye pia anaandikia gazeti la taifa la the Star,
alijizolea umaarufu mkubwa akiwa mtangazaji wa redio baada ya kujumuishwa
katika kutoa taarifa za michezo kila Jumatatu na Alhamisi kwenye kipindi
maarufu cha Mbusii na Lion Teketeke.
Katika mahojiano siku ya Jumatatu, Mballa na Uche waliahidi kuwapa burudani wasikilizaji wao."Tunataka kuwapa wasikilizaji tajriba ya kipekee, ambayo hawawezi kuipata popote pengine. Wale wanaofuatilia kipindi watafahamishwa na sasisho kwa wakati," alisema.
"Onyesho letu ni mchanganyiko wa kusisimua wa michezo na
muziki. Lengo letu kuu ni kuburudisha, kuelimisha na kuhabarisha,"
aliongeza.
"Tutacheza muziki bora zaidi wa hapa nchini, wa sasa na wa zamani. Zaidi ya kutangaza michezo ya ndani pia tunakusudia kukuza muziki wa humu nchini," Uche alisema.