
Mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi katika Radio Jambo Gidi Ogidi amemuomboleza kihisia mwanahabari mkongwe Leonard Mambo Mbotela.
Habari za kusikitisha za kifo cha mtangazaji huyo wa zamani wa redio zilisambaa kama moto wa nyikani Ijumaa asubuhi, na kuvunja mioyo ya wengi waliomfahamu.
Huku akimuomboleza, Gidi alizungumzia jinsi marehemu alivyochochea kazi yake ya utangazaji na akabainisha kuwa amehuzunishwa sana na habari za kifo chake.
“Nimesikitishwa sana kuskia hiyo habari kuhusu kifo cha mwenda zake,” Gidi alisema kwenye mahojiano ya simu.
“Huyu ni ndugu ambaye tumemfahamu sana, huyu ni ndugu ambaye nimelelewa nikimskiza kwenye redio. Ata mimi kuanza kazi yangu ya redio ni yeye alinivutia. Na miongoni mwa watu ambao nilikuwa najaribu sana kuiga kazi ambayo inafanana na yao kwenye redio ni Mzee Leonard Mambo Mbotela,” alisema zaidi.
Mtangazaji huyo mahiri wa kipindi cha asubuhi alizungumzia athari kubwa ya Leonard Mambo Mbotela katika tasnia ya habari nchini Kenya.
Pia alifichua jinsi nguli huyo maarufu kwa kipindi chake cha ‘Je, huu ni ungwana’ alivyokuwa akimpigia simu mara kwa mara ili kumtia moyo na hata kumrekebisha pale anapokosea.
“Ni huzuni sana kumpoteza gwiji wa redio
hapa nchini Kenya. Ni mtu ambaye alikuwa na historia nyingi kuhusu utangazaji
hapa nchini Kenya. Mara kwa mara alikuwa ananipigia simu. Ni mtu ambaye ata
katika uzee wake alikuwa akinipigia simu ananiuliza tunaendeleaje,
ananirekebisha, ananiambia leo niliskia ulisema hivi na kuwa hivi. Alikuwa
anafurahia sana, kwa hivyo ni huzuni sana kumpoteza mzee Leonard Mambo
Mbotela,” alisema.
Gidi alichukua fursa kumuomboleza marehemu Mbotela na kuwafariji familia, marafiki na mashabiki wake ambao wameguswa sana na taarifa hizo za kusikitisha.
“Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Tunaiombea familia yake, tunawaombea mashabiki wake, na kila mmoja ambaye alikuwa anamfahamu pale” alisema.
Mwanahabari mkongwe wa Kenya Leonard Mambo Mbotela alifariki dunia Ijumaa asubuhi.
Mkwe wake Anne Mbotela alithibitisha habari hizo za kusikitisha kwa Radio Jambo kupitia simu.
Mwanahabari huyo mkongwe alikuwa hajisikii vizuri kwa muda na alikata roho mwendo wa saa tatu unusu asubuhi siku ya Ijumaa.
"Ni kweli baba mkwe wangu amefariki," Anne alisema.