
Mwanahabari mkongwe Willy Michael Mwangi amemuomboleza mwenzake wa zamani na rafikiye wa muda mrefu Leonard Mambo Mbotela aliyeaga dunia Ijumaa asubuhi.
Habari za kusikitisha za kuaga dunia kwa Bw
Mbotela zilienea kama moto wa nyikani siku ya Ijumaa asubuhi na Mwangi amezungumza
kuhusu jinsi alivyohuzunika kumpoteza mwanamume anayemtambua kuwa kaka yake
mkubwa.
Akizungumza katika mahojiano maalum na radiojambo.co.ke,
Mwangi alizungumzia uhusiano wake wa karibu na marehemu Mbotela na jinsi
alivyokuwa sehemu ya kazi yake ya uandishi wa habari.
“Nachukua fursa kutuma rambirambi zangu kwa jamaa na marafiki wa marehemu, ndugu Leonard Mambo Mbotela. Marehemu, naweza kumuita kaka mkubwa maanake nilipojiunga na Voice Of Kenya ambayo sasa ni KBC mwaka wa 1983, ilikuwa tayari Leonard Mambo anafanya kazi pale,” Mr Mwangi alisema..
Mwanahabari huyo mkongwe alizungumza kuhusu kazi aliyofanya pamoja na Mbotela katika KBC, zamani ikiwa Voice Of Kenya, na jinsi alivyomfanya hata kuwa mtayarishaji wa kipindi cha Dunia Wiki Hii baada ya msimamizi wa awali kushindwa kufanya kazi hiyo kwa viwango vinavyohitajika.
"Leonard Mambo pia tumewahi kufanya kazi ya kipindi cha rais pamoja wakati wa kipindi cha hayati mtukufu rais Daniel Toroitich Arap Moi," alisema.
Pia alizungumzia uhusiano wake wa muda mrefu na wa karibu na familia ya marehemu Mbotela, na akafichua kwamba alisoma pamoja na marehemu Paulina Mbotela ambaye alikuwa kaka na mwenzake wa zamani.
Mwangi alifunguka jinsi habari za kuhuzunisha za kifo cha Mbotela zilivyomwacha na moyo uliovunjika.
“Kwa hiyo nimehuzunika sana na nilipopigiwa simu sikuwa na lolote la kufanya ila kukubali mambo ambayo ni ya mwenyezi Mungu. Tunasema kwamba mwenyezi Mungu, kazi yake haina makosa. Mimi nimehuzunika. Kwa niaba ya familia yetu yote tunatuma rambirambi wakati huu wa majonzi,” alisema.
Mwangi alisema amemfahamu Bw Mbotela tangu 1965 na amefanya kazi naye na kushirikiana naye katika mambo mengi.
“Nimemjua hayati Mambo Mbotela kwa muda mrefu. Na kifo chake ni pigo kubwa hussusan kwa sisi ambao tulianza kazi zamani miaka hiyo katika Voice of Kenya. Mola atulize jamaa yake, na marafiki kwa wakati huu na kuomba kila kitu kiende sawa,” alisema.
Marehemu Mbotela aliaga dunia Ijumaa asubuhi
baada ya kuugua kwa muda mrefu.