
Mtangazaji wa kipindi cha Gidi na
Ghost Asubuhi kwenye Radio Jambo, Jacob ‘Ghost’ Mulee amefunguka kuhusu harusi
ya hivi majuzi ya mwanawe Jesse Mutua na maelezo ya kipekee kuhusu binti mrembo
aliyemwoa.
Katika mahojiano ya kina na mtayarishaji wa maudhui, Samuel Maina, Ghost alifichua mambo ambayo hayakuwa yamejulikana na Wakenya wengi kuhusu mkwe wake mpya.
Ghost alieleza kuwa mkwe wake anatoka Mbalala, Uganda, kwa jamii ya Waankole.
“Kijana naye alienda mawindoni mpaka Uganda. Tulienda mpaka mji wa Mbalala kwa mahari, maana huyu mwanadada anatoka sehemu fulani ya huko. Ametoka kwa jamii ya Waankole,” Ghost alisema.
Mtangazaji huyo mcheshi alibainisha kuwa Jesse alikutana na mke wake wakati akisoma Uganda, na wamekuwa kwenye mahusiano kwa miaka kadhaa kabla ya kufunga ndoa wikendi iliyopita.
Hata hivyo, wawili hao walikuwa wakiishi tofauti kwani mamake Jesse, mke wa Ghost, alisisitiza kila kitu kifanyike kwa utaratibu unaostahili.
“Mpenzi wake ni mtu ambaye alikutana naye wakati akisoma kule Uganda. Walikutana kama wanafunzi miaka mingi iliyopita, na akaja akasomea hapa USIU. Wamekuwa wapenzi, lakini hawakuanza kuishi pamoja. Mamake, ambaye ni mke wangu, hapendi mambo ya mkato. Yeye anataka kila kitu kifanyike kwa mpangilio. Alimwambia kijana hawezi kuishi na msichana wa mtu kama wazazi wake hawajui,” alisema.
Ghost alizungumzia jinsi alivyokutana na babake binti huyo hapa Kenya kabla ya mipango ya harusi kuanza miaka miwili iliyopita.
“Babake (msichana) ni mtu wa kimataifa. Wakati alipokuja Kenya, tulipata fursa ya kushiriki chakula cha jioni pamoja na tukamwambia kwamba binti yake hajapotea Nairobi. Baada ya utambulisho huo, mipango ilianza rasmi. Tukaenda kufanya mambo ya mahari na taratibu zote, tukamaliza. Imekuwa safari ndefu ya takriban miaka miwili tukipanga harusi hii,” alisema.
Kocha huyo wa zamani wa Harambee Stars pia alifunguka kuhusu mila za wakwe wao na jinsi walivyorahisishiwa baadhi ya taratibu wakati wa maandalizi ya harusi.
“Wana taratibu na mila nyingi sana lakini nashukuru walitupunguzia. Kulingana na mila ya Waankole, tulihitajika kwenda Uganda mara saba kabla ya ndoa. Lakini kwa huruma yao, walipunguza na tulihitajika kwenda mara moja pekee kabla ya wao kuja Nairobi kwa harusi,” alisema.
Ghost alisema kuwa lilikuwa jambo la kujivunia sana kwake kuona mwanawe akifunga ndoa, baada ya kumlea tangu akiwa mtoto mdogo.
“Nilipokuwa kanisani, walipofunganishwa pale, nilijihisi kama kutoa machozi. Si kawaida yangu kulia lakini nilitoa machozi ya furaha nikikumbuka safari ya maisha ya kijana wangu tangu kuzaliwa kwake hadi sasa anapofunga ndoa,” alisema.