logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Ghost Mulee afunguka kuhusu tukio la kukatisha tamaa kwenye harusi yake miongo 3 iliyopita

Ghost amefunguka kuhusu jinsi siku yake ya harusi, zaidi ya miongo mitatu iliyopita, ilivyokaribia kuharibika.

image
na Samuel Mainajournalist

Mahojiano03 March 2025 - 13:27

Muhtasari


  • Ghost alieleza kuwa harusi yake ilifanyika kwa bajeti ndogo sana, tofauti na ile ya mwanawe ambayo ilifanyika wiki moja iliyopita.
  • Ghost alifichua kuwa kutokana na bajeti yao ndogo, baadhi ya maandalizi hayakufanyika vizuri.

Jacob 'Ghost' Mulee na mkewe Carol Mulee

Mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi katika Radio Jambo, Jacob ‘Ghost’ Mulee, amefunguka kuhusu jinsi siku yake ya harusi, zaidi ya miongo mitatu iliyopita, ilivyokaribia kuharibika..

Ghost alikuwa akilinganisha harusi ya mwanawe, Jesse Mutua, iliyofanyika hivi majuzi na harusi yake mwenyewe na mkewe Carol Mulee miaka mingi iliyopita, alipofichua tofauti kubwa kati ya hafla hizo mbili.

Akizungumza na mwanahabari Samuel Maina, mtangazaji huyo mwenye ucheshi alieleza kuwa harusi yake ilifanyika kwa bajeti ndogo sana, tofauti na ile ya mwanawe ambayo ilifanyika wakati ambapo waliweza kumudu vitu bora..

"Kuna tofauti kubwa kwa sababu wakati sisi tulifunga ndoa na mke wangu Carol, tulikuwa na matatizo mengi ya kifedha. Tulichangisha. Kutokana na hayo, tulikuwa tunafinya bajeti," Ghost alisema.

Kocha huyo wa zamani wa Harambee Stars alifichua kuwa kutokana na bajeti yao ndogo, baadhi ya maandalizi hayakufanyika vizuri, kwa mfano, hema la wageni kutumia katika karamu ya baada ya hafla ya harusi..

"Kitu kilinihuzunisha sana, mnamo siku ya harusi yangu na Carol, tulipokuja pale Impala ambako tulifanya hafla ya mapokezi, kuna jamaa alikuwa ametuagizia hema la sherehe ya harusi. Salaale! Tulipoteremka kutoka kwa gari, tuliona lile hema ni chafu kweli. Nikamwambia mke wangu, ‘unaona vitu vya bure vile vinavyokuwa’," alisema

Aliendelea kusema, "Sasa ilituudhi sana, lakini mimi wajua huwa sikasiriki, nilisema kama alileta chafu basi ilikuwa mpango ikuwe hivyo."

Ghost alisema, tofauti na harusi yake, harusi ya mwanawe iliyofanyika mwishoni mwa juma lililopita ilikuwa imepangwa vyema, na kila kitu kilikwenda sawa kama kilivyopaswa.

Alibainisha kuwa waliweza kumudu mipango yote ya harusi ya Jesse bila ya chochote kufeli.

"Kwa hii harusi ya kijana, mamake alihakikisha ameshughulikia maslahi ya kila kitu. Ilikuwa harusi ambayo ilienda kulingana na muda, ilikuwa na desturi nzuri, MC alifanya kazi yake vizuri. Kila mtu alijihisi kama yuko nyumbani na chakula kilikuwa kingi, ungerudia chakula mara kadhaa. Harusi ni chakula. Mtu akija harusi yako na asikule, atasema mpaka kifo. Tulihakikisha kila mtu alipata chakula cha kutosha," alisema.

Mtoto wa kwanza wa Ghost, Jesse Mutua Mulee, alifunga ndoa katika harusi ya kifahari iliyofanyika jijini Nairobi mwishoni mwa juma lililopita.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved