
Mwanadada aliyejitambulisha kama Ednah Mutheu (23) kutoka Machakos alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na aliyekuwa mpenzi wake, Albanus Wambua (30) ambye alikosana naye takriban miaka mitatu iliyopita.
Ednah alisema uhusiano wao wa mwaka mmoja ulivunjika Julai 2022 baada ya wazazi wake kukataa kuchukua mahari ambayo Wambua alitaka kupeleka nyumbani kwao ili amuoe.
Aidha, alifichua kwamba wakati alipopatana na Wambua, alikuwa na ujauzito wa mpenziwe wa awali ambaye alifariki.
“Tulipatana naye Facebook. Nikapata kumbe sio wa mbali sana na kwetu. Wakati huo nilikuwa katika chuo cha KMTC. Baby daddy wangu alipata ajali akafariki dunia,” Ednah alisimulia.
“Baada ya kupatana Facebook, akasema anataka bibi. Wakati huo sikumwambia niko na mimba. Nilikuja kumwambia baadaye baada ya kujuana. Hakukataa, alisema watoto tutapata. Wakati ukafika akasema anataka kupeleka mahari lakini wazazi wakakataa wakasema kwanza nimalize shule,” aliongeza.
Ednah alisema kwamba baada ya kumaliza shule hajaweza kuelewana na mpenziwe huyo kuhusu suala la ndoa.
“Sasa nimemaliza shule tayari. Nimekuwa nikimtafuta lakini anablock simu zangu. Kama ashamove ni sawa nitakubali, kama hajamove on nitamuomba msamaha juu nilimkosea. Mimi nilimuona ni jamaa mzuri ambaye ananipenda. Ata akinikataa ni sawa. Mtoto ako na miaka tatu, namshughulikia nyumbani,” alisema.
Wambua alpipogiwa simu, hakusita kueleza kwamba tayari amesonga mbele na maisha yake.
“Nilishamove on kitambo. Nilishamueleza. Alinipigia juzi akanisalimia tu,” Wambua alisema.
Ednah alisema, “Hakuniambia ashamove on. Aliniambia niende nimalize shule nitapata akiwa single.”
Hata hivyo, hakuwa na budi ila kukubali msimamo wa Wambua.
“Niko sawa, lakini sio sawa. Nilikuwa na matumaini lakini kama imekuwa hivyo ni sawa,” alisema.
Wambua alimwambia, “Namtakia mema kwa maisha yake.”