
Benson Andole, mwenye umri wa miaka 24, kutoka Kakamega
alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na baba mzazi wake Festus Muchesia (65)
ambaye alimtengana baada ya kukosana na mamake.
Benson alisema mzazi wake alimkana yeye na ndugu zake baada ya uhusiano wake na mama yao kukosana miaka mingi iliyopita.
Hii ilimlazimu kulelewa na nyanya yake hadi alipofariki akiwa kijana mdogo.
“Baba alikosana na mama yangu. Mzee alifika mahali akasema mimi sio mtoto wake. Alisema hatutaki juu amekosana na mama. Tulilelewa na nyanya yangu. Nyanya alipokufa alisema nirudi kwa boma. Baada ya kukaa na yeye mwaka moja akatufukuza. Nikasema niondoke nikarudi kwa momba wangu nikakaa huko. Ilifika mahali nikapata kazi,” Benson alisema.
Kijana huyo alisema angependa kurejesha uhusiano na mzazi wake ili kupata amani moyoni.
“Imefika mahali nikasema nataka amani. Kama ni shamba sitaki, nataka amani. Nataka tuwe kitu kimoja, kama ni vitu vingine nitatafuta mwenyewe. Ametenga dada yangu na pia kaka yangu wa huyo mama mwingine. Ametutenga wote,” alisema.
Bwana Festus alipopigiwa simu alimtaja mwanawe huyo kama mtoto
mtukutu, ambaye ni tofauti sana na ndugu zake.
“Kichwa yake ilikuwa tofauti. Nilitaka hata asome Polytechnic ikashindikana. Alikuja akanitusi, sikutaka hiyo maneno. Alinitukana mpaka anaandika meseji mbaya nikasema mimi sitaki,” Bw Festus alisema kabla ya kukata simu.
Benson alikanusha madai ya mzazi wake kwamba yeye ni mtukutu, na akasisitiza jinsi mzee huyo alivyomtenga.
“Alitufukuza nikiwa na mwaka mmoja. Kutoka wakati huo ni nyanya yangu alifunza hadi alipofariki. Mimi sikumtusi. Meseji nilimwandikia nilimwambia dadangu anasumbuka huku na asitutenge hadi kama alikosana na mama. Nikimpigia hawezi chukua simu. Mwaka jana aliita mama na mjomba akasema anataka kurejesha watoto wake hata kama alikosana naye,” alisema.
Bwana Festus alipigiwa simu tena lakini akaweka wazi kwamba hako tayari kurejesha uhusiano na mwanawe.
Benson alimalizia kwa kusema, “Baba mimi nakufahamu kama mzazi. Nilkuwa nataka Amani turejeshe mawasiliano, na pia niweze kupata baraka zako na niweze kusaidia ndugu zangu wakati nikiimarika.”
Je, una ushauri ama maoni gani kuhusu Patanisho ya leo?