
SIKU kadhaa baada ya kuibuka kwa uvumi kwamba lebo ya WCB Wasafi inaelekea kumuachilia msanii Mbosso kuondoka bila malipo hivi karibuni, bosi wa lebo hiyo, msanii Diamond Platnumz ametia neno kuhusu tetesi hizo.
Diamond alitoa tamko kupitia ukurasa wake wa Instagram akidokeza kwamba ni kweli kumefanyika mazungumzo na Mbosso kuhusu suala la kuondoka kwake lakini akaonya watu dhidi ya kueneza uvumi zaidi.
Diamond alisema kwamba suala hilo halifai kutanuliwa zaidi kwa njia yoyote ile hadi pale yeye au Mbosso watatoa tamko rasmi.
“Tumekuwa na mazungumzo mazuri na Mbosso namna ya kuanza rasmi sasa kusimamia kazi zake na tumekamilisha jambo letu vizuri sana. Tafadhali stori yoyote inayozungumzwa kuhusu jambo hili la Mbosso naomba zipuuzwe, mpaka mimi binafsi na Mbosso tutakapotoa tamko rasmi,” Diamond alisasisha.
Wiki jana, tetesi hizo zilitolewa na chawa wa Diamond na familia ya Wasafi, Baba Levo na kuzagaa kama moto wa nyikani.
Kulingana na Baba Levo, Diamond alikuwa amemruhusu Mbosso kuondoka bila kulipia chochote kama fadhila la kulipa utiifu wake katika muda wote ambao amekuwa chini ya lebo ya WCB Wasafi.
Baba Levo pia alibainisha kwamba WCB Wasafi ilikuwa imeanzisha mchakato wa kuwasaini wasanii wengine 9 kuchukua nafasi ambayo imeachwa na kuondoka kwa Mbosso na watangulizi wake – Harmonize, Rayvanny, Queen Darleen na Rich Mavoko.
“Kutokana
na heshima kubwa ya Mbosso kwa Diamond na viongozi wa WCB, Lukuga [Diamond]
amemfungulia milango Mbosso akajitafutie mwenyewe bila kulipa chochote WCB.”
“Nidhamu Kubwa Ya MBOSSO Imemfanya @diamondplatnumz Amsemehe MAMILIONI YA PESA Na Kumpa UHURU WA KWENDA KUPAMBANA NNJE YA WCB,” Baba Levo aliakisi.
Hata hivyo, baada ya Diamond kutoa tamko rasmi na kuwafunga midomo baadhi ya waliokuwa wakieneza tetesi hizo nje ya muktadha, Baba Levo mwenyewe alirudi mtandaoni na kubadili msimamo wake kama muasisi wa taarifa zenyewe.
Levo alisema kwamba alinukuliwa vibaya na hata kudai kwamba uvumi huo haukutoka kwake bali ni mtu alimuiga kwa kutumia Teknolojia ya akili mnemba, AI.