
WAZIRI wa Ardhi, Alice Wahome amekutana na mchungaji James Maina Ng’ang’a wa kanisa la Neno Evangelism, siku kadhaa baada ya pasta huyo kumfukuza mwanamke kanisani na kumtaka kutafuta usaidizi wa serikali.
Katika chapisho lake kupitia ukurasa wa Facebook, CS Wahome
alifichua kwamba Ng’ang’a alimtembelea katika ofisi yake kujadili masuala ibuka
kuhusu mradi wa serikali wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu.
“Asubuhi ya leo, Mtume
James Maina Ng’ang’a amenitembelea kwa ukarimu ili kujadili Mpango wa Serikali
wa Nyumba Nafuu. Ushirikiano huu ni sehemu ya juhudi zetu zinazoendelea za
kuelimisha na kujenga ufahamu miongoni mwa Wakenya kuhusu fursa zinazopatikana
kupitia mpango huu wa kuleta mabadiliko,” Wahome alisema.
Waziri huyo alisema kwamba mchungaji Ng’ang’a alikuwa na uchu
wa kutaka kujua jinsi mradi wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu unaonyesha kuongezeka
kwa uelewa na msaada kutoka sekta mbalimbali za jamii.
“Ziara ya Mtume Ng’ang’a
ni ya kutia moyo na yenye athari. Nia yake ya kuelewa programu inaonyesha
kuongezeka kwa ufahamu na usaidizi kutoka kwa sekta mbalimbali za jamii. Wakati
wa majadiliano yetu, nilijitolea kumwongoza katika mchakato wa kupata nyumba za
bei nafuu na kumfundisha kuhusu muundo na manufaa ya program,” CS Wahome alisema.
Waziri alisema lengo la serikali ni kujenga nyumba takribani
milioni moja katika kipindi cha miaka 5 ijayo.
“Lengo letu ni kubwa
lakini linaweza kufikiwa: kutoa nyumba milioni 1 katika miaka mitano ijayo, na
kufikia zaidi ya Wakenya milioni 15 moja kwa moja na kwa njia zisizo za moja
kwa moja,” alisema.
Mkutano wao umetokea wiki chache baada ya Ng’ang’a kusutwa
kwa kumfukuza Milka Moraa Tegisi kanisani na kumtaka kuenda kwa serikali
kutafuta msaada baada ya kuomba msaada wa kodi ya nyumba.