
MSHAWISHI mwenye misimamo mikali dhidi ya hulka mbalimbali za binadamu kwenye mitandao wa X, Eric Amerix ameibuka na maoni yake kuhusu siku ya wapendanao.
Siku ya Wapendanao, au valentine huadhimishwa katika mataifa
mengi duniani mnamo Februari 14 lakini kwa Amerix, siku hiyo haina maana
yoyote, haswa kwa wanaume.
Amerix, ambaye mara kwa mara huibuka kama mtetezi wa wanaume
na kuwaonya dhidi ya kile anachokiita kuwa dhana za kike alisema kwamba siku ya
wapendanao huwavutia sana wanawake na mwanamume kamili hafai hata kuvutiwa na
chochote kuhusu Februari 14.
Kwa mujibu wake, Siku ya Valentino ni ya wanawake pekee na
kama kuna mwanamume anayevutiwa nac siku hiyo basi huyo ni wa kujipendekeza tu.
Aliwashauri watu kutumia fedha zao katika kufanyia maendeleo
yenye tija kama kukodisha shamba na kufanya ukulima badala ya kuzitumia katika
kununua zawadi kwa ajili ya kuwapa wanaowapenda.
“PINGA mwelekeo wa mvuto karibu na siku ya VALENTINE. Jiweke mbali na obiti hii ya kimatumizi ya wanawake. Hifadhi rasilimali zako. AU, Tumia rasilimali hizo kukodisha ardhi na kupanda mboga. Siku ya wapendanao ni ya simps & orbiters,” Amerix alisema.
‘Simp’ ni neno la lugha ya mtandaoni linaloelezea mtu ambaye
anaonyesha huruma na umakini kupita kiasi kwa mtu mwingine, kwa kawaida kwa mtu
ambaye harudishi hisia zile zile, katika kutafuta mapenzi au uhusiano wa
kimapenzi.
Kwa upande mwingine, ‘Orbiter’ ni kitu au kifaa ambacho kazi
yake ni kuzunguka tu kando kando ya chombo Fulani badala ya kutua kwenye chombo
hicho.
Maoni ya Amerix yanakuja wakati ambapo nchini Kenya watu
wanasherehekea siku hii kwa kuwatunuku wale wanaowapenda.
Siku hii huadhimishwa na rangi ya waridi ambapo watu
huzawidiana maua ya rangi ya waridi, pipi, chokoleti na vitu vingine.
Hata hivyo, humu nchini, kuna dhana ambayo imejikita kwenye
fikira za wengi kwamba Valentino ni siku ya kuwazawadi wanawake tu na kwamba
wanaume hawafai kupokea zawadi haswa kutoka kwa wanawake.