
MKURUGENZI Mtendaji katika Shirika la Hakimiliki ya Muziki ya Kenya (MCSK), Dkt Ezekiel Mutua amezua maswali kuhusu mmomonyoko wa maadili nchini Kenya haswa kwa kizazi cha sasa.
Kupitia ukurasa wake wa X, Mutua alihoji ni
vipi jamii ya sasa imefika mahali ambapo wanamchukia mtu aliyekufa bila kujali
msemo wa kale wa ‘Marehemu hasemwi vibaya’.
Mutua alisema kwamba kizazi cha sasa hakina
huruma na heshima kwa marehemu kiasi kwamba hata katika umauti wao, bado
wanazidi kumtakia tu kifo bila kujali kwamba ameshakufa.
“Ilikuwaje tukapotoka kimaadili hadi
kuwasema vibaya wafu, tuwachukie watu hadi kuwatakia kifo hata wakiwa wamekufa?” Mutua alihoji.
Mutua alisema kwamba jambo hilo lilimuacha
akifikiria sana alipoona watu wakimsema vibaya aliyekuwa mwenyekiti wa tume ya
IEBC, Wafula Chebukati baada ya taarifa za kifo chake.
Alisema kwamba alisikia maoni hayo
yakifokwa katika hafla moja ambayo kinara wa chama cha DAP-K, Eugene Wamalwa
alikuwa amehudhuria baada ya kutoa ramirambi zake kwa mwendazake Chebukati.
“Nilikumbana na matamshi ya
kusikitisha katika hafla iliyohudhuriwa na aliyekuwa Waziri Eugene Wamalwa
ambaye alikatizwa na nyimbo za "Wacha akufe tu" alipotaja kuwa
tumempoteza aliyekuwa Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati. Tumepoteza ubinadamu
wetu? Tutaipataje tena kama nchi?” Mutua
aliuliza zaidi.
Kifo cha Chebukati kulihuzinisha taifa
Ijumaa asubuhi baada ya familia yake kutangaza kwamba alikuwa amekufa usiku
uliopita wakati wa akipokea matibabu hospitalini.
Hata hivyo, familia iliomba kupewa faragha
yao wanapomuomboleza mpendwa wao.
Chebukati alichukiwa na kupendwa kwa
viwango sawa haswa kutokana na utendakazi wake akiwa mwenyekiti wa tume ya IEBC
kati ya 2017 na 2022.