
Mchekeshaji David Oyando maarufu Mulamwah ametangaza kuondoka kwenye kazi ya radio katika kampuni ya Media Max baada ya takribani miaka mitatu.
Wakati akitoa tangazo hilo kwenye mtandao wa Instagram, alieleza kwamba mkataba wake ulikuwa umeisha na hakuafikiana na wasimamizi kuhusu mkataba mpya.
"Mwisho wa show Konki. Ninaondoka. Imekuwa safari nzuri. Mwishowe, tumekamilisha mahusiano na stesheni ya Milele na kampuni ya Media max. Mkataba umekamilika na hatujakubaliana kuhusu swala la mkataba mpya," Mlamwah aliandika kwenye instagram Jumanne.
Mchekeshaji huyo aliwatakia wenzake kila la heri wakati akitangaza kuondoka, pia ameupongeza usimamizi na kueleza kwamba amejifunza mengi. Aliongeza kwamba wafuasi wake ambao wamekuwa wakimfuatilia bado watakutana naye kupitia majukwaa mengine.
"Shukrani kwa wenzangu na usimamizi kwa ajili ya miaka hii ya kazi nimepata uzoefu na nimejifunza mengi. Kwa wafuasi wangu wa konki tutakutana kwa majukwaa mengine," alidokeza.
Alielezea kwamba kuna mipango mingi ambayo inaendelea kujiri ikiwa ni pamoja na kufungua jukwaa lingine la Youtube.
Mulamwah alijiunga na stesheni hiyo mnamo Mei 16 2022 na amekuwa huko kwa muda wa karibu miaka mitatu..