

MCHUNGAJI wa kanisa la New Life Prayer Centre lililoko Mavueni kaunti ya Kilifi amejitokeza kimasomaso kutetea hatua ya rais William Ruto kutoa mchango wa shilingi milioni 20 katika kanisa moja kaunti ya Kiambu wiki jana.
Katika moja ya video za mahubiri yake ambayo imevutia hisia
mseto ambapo alisema rais hujafanya lolote baya kutoa pesa hizo kwa ajili ya
maendeleo ya kanisa.
Hii inajiri wakati ambapo rais Ruto amekuwa akikosolewa kwa
kutoa mchanga wa shilingi milioni 20 katika kanisa la Jesus Winners Ministry
wikendi iliyopita
Kwa mujibu wa Ezekiel, rais Ruto ni mtu mwenye pesa zake na
hakukosea mtu yeyote kwa kutoa kiasi hicho kikubwa cha mchanga kanisani.
“Rais Ruto hana ndege?
Helikopta si alikuwa anakampeni nazo? Huyu mtu atakuwa rais na hana pesa? Akitoa
pesa zake aende akatoe sadaka, amekukosea? Acheni tabia mbaya nyinyi. Tuache hii
tabia ya kukashifu kila kitu,” Ezekiel alisema huku akifichua kwamba
alijua atazua gumzo baada ya kumkingia Ruto kifua.
Ezekiel aliendelea kumtetea Ruto dhidi ya dhana kwamba
milioni 20 alizotoa kanisani ni za ufisadi, akisema kwamba mkuu wa nchi kando
ya mshahara wa milioni 2, yeye ni mfanyibiashara mkubwa.
“Wewe unataka kuniambia
rais Ruto hana pesa? Unataka kuniambia zile milioni 2 mnamlipa kama mshahara
ndio pesa anategemea? Hapana… eti sasa akitoa 20m ni habari?”
Ezekiel alisema kwamba yeye amewahi fungwa na hii serikali –
akirejelea masaibu yake miaka miwili iliyopita kutokana na matukio ya Shakahola
– lakini akisema kwamba mahali ataona wananchi wanakosea sharti atawaambia.
“Hapo mnamkosea rais. Akitoa milioni 2 mnarudisha akitoa 5m mnarudisha na akitoa elfu 50 mtaanza kusema hiyo ni pesa gani rais mzima anatoa. Hapana. Kama mnachukia mtu mchukie yeye binafsi lakini msichukie urais,” Ezekiel alisisitiza.
Mchungaji huyo aliwarai waumini wake kutomchukia mtu ambaye
anawapa chakula na kukitupa wakati hawana chakula chenyewe.
Licha ya kukosolewa vikali, rais Ruto pia amekuwa akipata
watetezi ambao wamesimama kidete kutetea sadaka yake kanisani.
Kanisa katoliki limekuwa katika mstari wa mbele kumkosoa Ruto
kwa pesa anazotoa kanisani.