
Jenerali Muhoozi Kainerugaba, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Uganda (UPDF) na mwana wa Rais Yoweri Museveni, amefichua sababu tata inayomfanya kuepuka kuhudhuria ibada za kanisa.
Kupitia jumbe zake za Jumanne asubuhi, Muhoozi alieleza kuwa yeye huomba akiwa kambini na wanajeshi wake badala ya kanisani.
Sababu kuu ya hili, anasema, ni uwepo wa wanawake warembo kanisani ambao anaamini ni majaribio makubwa kwake.
"Ndiyo maana ninaepuka ibada za kanisani kwa makusudi. Kuna wanawake wengi warembo sana huko. Ni kama shetani anawaleta wote kwa ajili yangu. Hapana, mimi huomba kambini na wanajeshi wangu. Huko tunaweza kumlenga Mungu kikamilifu!" aliandika Muhoozi kwenye akaunti yake ya Twitter.
Kauli yake ilikuja baada ya mwanawe Museveni kudai kwamba kuwa mwanajeshi ni moja ya uamuzi bora kwa mwanaume, lakini akasisitiza kuwa hatua bora zaidi ni kuwa padre—kumtumikia Mungu kikamilifu.
Hata hivyo, alisema kwamba yeye hawezi kuwa padre kwa sababu hana uwezo wa kuachana na wanawake na kumlenga Mungu pekee.
"Zamani nilisoma mahali kwamba kuwa mwanajeshi ni jambo la pili bora zaidi kwa mwanaume. Jambo bora kabisa ni kuwa padre, kumtumikia Mungu kwa moyo wote, kuachana na wanawake na kumlenga Mungu pekee. Niliposikia suala la kuachana na wanawake, nilijua siwezi," alisema.
Muhoozi, ambaye anajulikana kwa kauli zake tata kwenye mitandao ya kijamii, alijivunia kuwa na wafuasi wengi wa kike, akiwataja kama viumbe warembo zaidi walioumbwa na Mungu.
Pamoja na hayo, alihimiza vijana wa Uganda na Afrika kwa ujumla kujiunga na jeshi ili kufurahia faida za maisha ya kijeshi.
"Kwa vijana wa Uganda na Afrika, huwezi kuwa mwanaume kamili kama hujawahi kuhudumu jeshini. Hilo haliwezekani," alisisitiza.
Muhoozi alifafanua kuwa ili mtu ajiunge na jeshi la Uganda, anahitaji kuwa na afya njema, kuwa raia wa Uganda, kuwa na nidhamu na elimu inayohitajika.
"Kama kuna afisa wa UPDF anayekutaka utoe pesa ili akuajiri, niambie jina lake hapa na ataona cha mtema kuni," alionya.
Muhoozi ameendelea
kuvutia mijadala kutokana na matamshi yake yenye utata kwenye mitandao ya
kijamii, huku wengine wakimtazama kama mrithi wa baba yake katika siasa za
Uganda.