
Luteni Jenerali Muhoozi Kainerugaba, mwanawe Rais wa Uganda Yoweri Museveni, amezua mjadala mkali kwenye mitandao ya kijamii baada ya kudai kwamba ameua maadui 30,000 katika taaluma yake ya kijeshi.
Kauli hii, iliyotolewa kupitia mtandao wa X (zamani Twitter), imeibua maswali mengi kuhusu athari za matamshi yake, hasa ikizingatiwa kuwa yeye ni mmoja wa maafisa wa juu katika jeshi la Uganda.
Katika ujumbe wake, Muhoozi alijieleza kwa njia inayoonekana kuwa ya dhihaka, akidai kuwa idadi hiyo ni ndogo kulinganisha na matarajio yake.
"Katika taaluma yangu ya kijeshi, nimefanya vibaya. Nafikiri nimeua tu maadui 30,000. Utendaji kazi mbaya sana," Muhoozi aliandika Ijumaa jioni.
Pia, alionekana kujilinganisha na aliyetaja kuwa mjomba wake Afande Paul, akisema anatamani kufanya vizuri zaidi ya yeye katika masuala ya kijeshi.
"Nataka kufanya vizuri au hata zaidi ya mjomba wangu Afande Paul." alisema.
Matamshi haya yamepokewa kwa hisia tofauti, huku wengine wakiyatafsiri kama kejeli, wakati wengine wakiyachukulia kama kauli za hatari kutoka kwa kiongozi wa kijeshi.
Huku matamshi yake ya idadi ya vifo yakizua mshtuko, Muhoozi pia ameendelea kuzungumzia siasa za Kenya kwa njia tata.
Katika moja ya jumbe zake, alidai kuwa Kenya ni nyumbani kwake na hata akaenda mbali zaidi akitangaza kuwa atagombea nafasi ya ubunge katika eneo la Westlands, Nairobi, mwaka wa 2027.
"Naam, mnafikiri ni mzaha? Mwaka wa 2027 ninasimama kugombea ubunge kutoka Nairobi! Wakenya wangu waanze kunipigia kampeni!" alisema Muhoozi, jambo lililozua mshangao na maswali mengi kuhusu uhalali wa azma yake, ikizingatiwa kuwa yeye si raia wa Kenya.
Katika ujumbe mwingine, alionekana kuwakejeli wanaume wa Kenya kwa kusema: "Unaweza kujua jinsi wanaume wanavyoweza kupiga risasi kulingana na unyoofu wa pua zao. Pua za wanaume wa Kenya ziko ovyo ovyo. Ndiyo maana wanawake wao wamekata tamaa."
Kauli hizi zimeibua hisia kali mtandaoni, huku baadhi ya watu wakiziona kama mzaha wa kawaida wa Muhoozi, wakati wengine wakiziita kejeli na uchokozi dhidi ya Kenya.
Hii si mara ya kwanza kwa Muhoozi kutoa matamshi yanayozua utata. Mwaka wa 2022, alidai kuwa jeshi lake lingeweza kuteka Nairobi kwa muda wa wiki mbili, jambo lililozua mtafaruku wa kidiplomasia kati ya Kenya na Uganda.
Licha ya kauli zake za mara kwa mara zinazolenga Kenya, Muhoozi anaonekana kujiimarisha kisiasa nchini Uganda, huku wachambuzi wakihisi kuwa anatumia mitandao ya kijamii kujitengenezea jina kwa lengo la kumrithi baba yake kama rais wa Uganda.
Hadi sasa, hakuna tamko rasmi kutoka kwa serikali ya Uganda au Kenya kuhusu matamshi yake ya hivi karibuni.