logo

NOW ON AIR

Listen in Live

"Inaniumiza!" Rais Yoweri Museveni Ashangazwa na Umaskini nchini Uganda

Museveni ameeleza masikitiko yake kuhusu hali ya umaskini inayoendelea kuwakumba wananchi wa nchi yake.

image
na Samuel Mainajournalist

Kimataifa26 February 2025 - 11:21

Muhtasari


  • Museveni alisema amekuwa akihamasisha Waganda kuhusu njia za kujikwamua kiuchumi kwa miaka mingi, lakini bado baadhi yao wanaonekana kushindwa.
  • Museveni aliwaambia wananchi kuwa serikali iko tayari kuongeza fedha za PDM kwa familia zinazoonyesha maendeleo.

Uganda President Yoweri Museveni/FILE

Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, ameeleza masikitiko yake kuhusu hali ya umaskini inayoendelea kuwakumba wananchi wa nchi hiyo jirani, akisema kuwa ni jambo linalomuumiza licha ya juhudi za serikali za kuboresha maisha yao.

Akizungumza katika ziara yake ya kukagua utekelezaji wa mpango wa maendeleo vijijini (Parish Development Model - PDM) katika eneo la Ankole, Museveni alisema kuwa amekuwa akihamasisha Waganda kuhusu njia za kujikwamua kiuchumi kwa miaka mingi, lakini bado baadhi yao wanaonekana kushindwa kuondokana na hali hiyo.

Serikali ya Uganda ilizindua mpango wa Parish Development Model (PDM) mwaka 2022 kama mkakati wa kusaidia familia masikini kuboresha maisha yao kupitia mikopo nafuu na miradi ya kujiongezea kipato. Kila familia inayofuzu kupata msaada huo hupokea kiasi cha Shilingi milioni moja za Uganda, ambazo zinapaswa kutumiwa kwa shughuli za uzalishaji mali.

Katika hotuba yake, Rais Museveni alisisitiza kuwa fedha hizo zitatolewa kila mwaka kwa walengwa, lakini ni jukumu la wananchi kuhakikisha kuwa wanazitumia kwa njia sahihi ili kufanikisha lengo la kupunguza umaskini. Alitoa mfano wa Bi Tumusiime Deziranta, mmoja wa wanufaika wa mpango huo, ambaye ameweza kuboresha maisha yake kupitia ufugaji wa nguruwe na mbuzi baada ya kupokea msaada wa serikali.

Museveni aliwaambia wananchi kuwa serikali iko tayari kuongeza fedha za PDM kwa familia zinazoonyesha maendeleo, lakini akasisitiza kuwa ni lazima watu wajitume zaidi na kuchukua hatua za kubadilisha hali zao.

"Najua umaskini ni tatizo lenu binafsi, lakini mimi kama kiongozi wenu, inaniumiza kuwaona mkiendelea kuteseka. Fedha hizi tunazowaletea ziwasaidie kuinuka kiuchumi, na kwa wale watakaotumia vizuri, tutahakikisha wanapata nyongeza ili kuendelea kuboresha maisha yao," Museveni alisema Jumanne.

Kwa mujibu wa takwimu, takriban asilimia 40 ya Waganda bado wanaishi chini ya mstari wa umaskini, huku wengi wao wakiendelea kukabiliwa na matatizo ya msingi kama ukosefu wa chakula, huduma za afya, na elimu bora.

Serikali inatarajia kuwa kwa kushirikiana na wananchi, miradi kama PDM inaweza kusaidia kuinua hali ya maisha ya Waganda na kuimarisha maendeleo ya kiuchumi nchini Uganda. Swali linalobaki ni ikiwa wananchi watatumia ipasavyo fursa hii au wataendelea kushikilia hali yao ya sasa.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved