
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi wa Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, mnamo siku ya Jumapili alitangaza kuwa yeyote atakayepatikana akiwa amevaa mavazi ya Chama cha National Unity Platform (NUP) atauawa.
Kupitia chapisho lake kwenye mtandao wa X, Muhoozi, ambaye ni mwanawe Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, alitoa onyo kali akisema kuwa kuanzia sasa, yeyote atakayekamatwa akiwa amevaa sare za NUP atauawa bila kusita.
NUP ni chama cha upinzani nchini Uganda na kinaongozwa na aliyekuwa Mbunge wa Kyadondo, Robert Kyagulanyi Ssentamu, al maarufu kama Bobi Wine.
“Kuanzia sasa, tukimkuta mtu yeyote amevaa sare za NUP, tutamuua! Hakuna maswali!” aliandika Muhoozi.
Hata hivyo, matamshi hayo yenye utata yamefutwa tangu yalipochapishwa.
Tamko hili tata linakuja baada ya kusambaa kwa video inayoonyesha wanachama wa NUP wakifanya gwaride katika makao makuu ya chama chao kwa mtindo ambao jeshi la Uganda linadai inafanana na mazoezi ya kijeshi.
Tangu video hiyo ilisambaa, wanachama kadhaa wa NUP wameripotiwa kutoweka, akiwemo mkuu wa uhamasishaji wa chama, Fred Nyanzi, ambaye alipotea kwa siku kadhaa kabla ya kuonekana tena.
Wiki iliyopita, kulikuwa na ripoti nyingi za uvamizi wa kijeshi dhidi ya wanachama wa NUP, ambao hujulikana kama “Foot Soldiers” na huvaa mavazi mekundu, rangi ambayo jeshi la Uganda linadai inafanana na sare zao.
Gwaride hilo pia lilisababisha vikosi vya usalama kuvamia ofisi za chama, huku polisi wakidai kuwa mazoezi ya kijeshi yasiyoidhinishwa yalikuwa yakifanyika katika maeneo ya NUP.
“Kufuatia ripoti za mazoezi ya kijeshi yasiyoidhinishwa katika makao makuu ya National Unity Platform (NUP) huko Kavule na katika ofisi yao iliyopo Kamwokya, Kampala, Jeshi la Polisi la Uganda, kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama, limeanzisha operesheni ya pamoja ya kiusalama. Maafisa wetu wa usalama kwa sasa wanafanya msako katika maeneo yaliyotajwa. Taarifa zaidi kuhusu matokeo ya operesheni hii zitolewa baadaye,” alisema msemaji wa polisi, Kituuma Rusoke, wiki iliyopita.
Katika tamko lingine, Muhoozi alitaja mazoezi ya wanachama wa NUP kuwa haramu na akaongeza vitisho vya kuwaua wale watakaoshiriki katika shughuli hiyo tena.
“Hili ni kosa kisheria! Na waendelee kulifanya tena, tuone nani ataendelea kuwa hai,” aliandika kwenye X.
Katika majibu yake, kiongozi wa NUP, Robert Kyagulanyi, alilaani uvamizi wa ofisi za chama chao, akisema ni ukiukaji wa haki zao unaoendelea.
Pia alielezea wasiwasi wake juu ya matamshi ya Muhoozi na kuwataka walimwengu wasipuuze kinachoendelea nchini Uganda.
“Watu wengine hutushauri tusijali matamshi ya mtoto mkatili wa Museveni, wakiyachukulia kama maneno ya mlevi. Lakini ukweli ni kwamba mtoto wa Museveni ndiye mkuu wa jeshi letu—hata kama alipewa nafasi hiyo kinyume cha sheria na baba yake. Ana uwezo wa kutekeleza vitisho vyake, na tayari ameanza,” alisema Bobi Wine.
Aliongeza, “Utekaji nyara, mateso na uvamizi wa wiki hii ni uthibitisho wa kile anachoweza kufanya. Tunapoendelea kuhamasisha na kuwataka watu wetu kupambana na hawa wahalifu, DUNIA ISIPUUZE KINACHOENDELEA UGANDA. Utawala huu, ambao uko katika hatua zake za mwisho, umepoteza mwelekeo kabisa.”