
Luteni Jenerali Muhoozi Kainerugaba, mtoto wa Rais Yoweri Museveni na mmoja wa viongozi wakuu wa jeshi la Uganda, ameibua mjadala mpya baada ya kumwomba aliyekuwa rais wa Marekani, Donald Trump, kusaidia kurejesha msaada wa dawa za Ukimwi kwa waathiriwa katika taifa hilo jirani.
Katika ujumbe wake wa Jumapili jioni, tarehe 2 Machi 2025, kwenye mtandao wa X , Muhoozi alimtag Trump moja kwa moja, akieleza kuwa msaada wa Marekani kwa wagonjwa wa Ukimwi nchini humo ni wa umuhimu mkubwa na kwamba watu wa Uganda watafurahia ikiwa utarejeshwa.
"Nataka kumuomba Rais @realDonaldTrump arejeshe msaada wa Marekani kwa waathiriwa wa Ukimwi Uganda. Watu wetu watashukuru," Muhoozi alisema.
Hatua ya mwanawe Museveni inakuja baada ya Rais Donald Trump kusitisha ghafla misaada ya kigeni, ikiwemo ile ya USAID na mpango wa PEPFAR (President’s Emergency Plan for AIDS Relief).
Misaada hii ilikuwa msaada mkubwa katika mapambano dhidi ya Ukimwi, haswa katika nchi zinazoendelea kama Uganda.
Kwa miaka mingi, Uganda imekuwa ikitegemea PEPFAR, ambapo Marekani ilitoa mabilioni ya dola kugharimia dawa za kupunguza makali ya Ukimwi (ARV).
Hata hivyo, utawala wa Trump umepunguza au kusitisha misaada hiyo kwa baadhi ya mataifa, akitaja sababu kama "marekebisho ya sera za misaada ya nje."
Kusitishwa kwa misaada ya Marekani kumeleta madhara makubwa kwa waathiriwa wa Ukimwi nchini Uganda.
Kwa mujibu wa ripoti ya Al Jazeera, vifo vinavyohusiana na Ukimwi barani Afrika vinatarajiwa kuongezeka kwa sababu wagonjwa wengi wanashindwa kupata dawa za ARV.
Uganda inakadiriwa kuwa na zaidi ya watu milioni 1.4 wanaoishi na VVU, na wengi wao walikuwa wakitegemea msaada wa PEPFAR.
Mashirika ya afya yanasema kuwa vituo vya afya vimepungukiwa na rasilimali, na hali hii inahatarisha mafanikio yaliyopatikana katika vita dhidi ya Ukimwi.
Muhoozi, ambaye amekuwa akimsifu Trump mara kwa mara, anaonekana kutumia uhusiano huo kujaribu kushawishi kurejeshwa kwa msaada wa dawa za Ukimwi.
Hata hivyo, haijulikani kama Trump atakubali ombi hilo, hasa ikizingatiwa kuwa alishapunguza misaada mingi ya afya katika muhula wake wa kwanza.
Wakati huu ambapo waathiriwa wa Ukimwi wanazidi kuhangaika, bado haijulikani ikiwa hatua yoyote itachukuliwa kurekebisha hali hii.