
MCHAMBUZI wa masuala mbalimbali ya kijamii, Cassypool amefichua kwamba ukaribu wake na rais William Ruto una mnato wa kipekee kiasi kwamba akitaka kazi ya serikali haitomchukua zaidi ya dakika moja.
Akizungumza na waandishi wa habari za burudani, Cassypool
alisema kwamba kwa wakati mmoja Ruto aliwahi kumpa kazi serikalini lakini
akaikataa.
Hata hivyo, uhusiano wake na kiongozi wa nchi bado ungali na
mashiko ya kipekee, akifutilia mbali kwamba urafiki ulisambaratika ndio maana
hajaonekana ikuluni katika siku za hivi karibuni.
Alisisitiza kwamba rais Ruto ni mmoja kati ya watu wangwana
sana kukutana nao na kusema leo hii akaamua kutaka kazi serikalini ni kunyanua
simu moja tu na chini ya dakika nzima kazi anayo.
“Nilikuwa na rais William
Ruto kwenye ikulu na mliona kwenye mitandao ya kijamii. Kama kuna rais ambaye
ni muungwana, rais ambaye ni mstaarabu ni William Samoei Ruto.”
“Mimi nikitaka leo hii
kazi ya serikali hii nchi, haiwezi nichukua zaidi ya dakika moja kupiga simu na
kupata kazi ya serikali. Kama kuna kitu siwezi hangaika kupata ni kazi ya
serikali,” Cassypool alijigamba.
Lakini je, ni kipi ambacho kinamzuia kutopiga simu na kuwahi
hiyo kazi?
Kwa mujibu wake, kazi za serikali zina taratibu zake maalum
ambayo kwa njia moja au nyingine zinamkalia vigumu kuziendea.
“Lakini kazi ya serikali
iko na taratibu ya kwanza huwezi kufanya siasa, huwezi kupiga mbwebwe, huwezi
kusafiri kwenda Tanzania kufanya siasa tena Tanzania ama kufanyia serikali ya
kule kazi kwa sababu wewe ni mwajiriwa wa serikali.”
“Sasa mimi niko
passionate kuhusu mama Samia Suluhu nataka yeye ashinde muhula mwingine wa
urais mwezi Oktoba na mimi ni influencer kutoka Kenya. Hivyo mimi siwezi
kuchukua kazi ya serikali [ya Kenya] kama nampigia debe Samia, kwa sababu itanifungia
kusema mema na mazuri maana kuna kanuni za serikali huwezi kuenda kuzungumzia
vitu tofauti,” alieleza.
Alitaja ukuruba wake na rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan
kama sababu iliyomfanya kukataa kazi ya serikali ya Kenya kutoka kwa William
Ruto.