
CASSYPOOL amejiunga na Weezdom kukejeli kolabo mbili zilizoachiliwa na wasanii Bahati na Willy Paul baada ya kujenga upya urafiki wao.
Akizungumza na mtengenezaji wa maudhui Trudy Kitui, Cassypool alisema kwamba hakuna msanii wa Kenya anaweza faulu kwa kuimba jinsi wawili hao wanaimba.
Kwa mujibu wa Cassypool, ngoma za ‘Keki’ na ‘Paah’ zilizofanywa kikoa na Bahati na Willy Paul na kuachiliwa Ijumaa iliyopita si kingine zaidi ya takataka.
Cassypool alisema kwamba wawili hao wanajaribu kuimba Watanzania katika uimbaji, kitu ambacho kinakwamisha ngoma zao kutoka katika ubora unaostahili.
“Mimi nilisema huwezi kuimba kama Mbongo na uhit. Haiwezekani. Unaimba kama Diamond na unataka ku’hit eti tukuje tukusifiwe eti umetoa ngoma kubwa. Hiyo ni kuharibu wakati; ni takataka. Ni nini hiyo waliimba?” Cassypool alisema.
Kwa mujibu wa Cassypool, ngoma za wawili hao haziwezi kuwa pendwa kwa mashabiki wengi zaidi ya wiki moja kwa sababu zinaiga ladha za kigeni.
Cassypool aliipigia chapuo Gengetone na Arbantone kwamba ndizo zitateka anga za mawimbi ya muziki wa Kenya kwani nfizo ngoma zenye ladha halisi ya humu nchini.
“Huwezi kuimba ngoma ambazo zina’hit kwa wiki moja tu. Gengetone ndio inateka anga. Lakini ukituwekea vijana wawili mmoja amebeba kifua mawe yamelala upande mmoja na kifua imelala huku kwingine halafu mwingine anaimba kwa sauti ya soprano kama mwanamke na kutuambia hao ndio wasanii ni kazi bure,” Cassypool alisema.