
TIKTOKER Rachel Otuoma amefunguka jinsi penzi lake na marehemu mwanasoka Ezekiel Otuoma bado lingalipo licha ya kumzika mwanasoka huyo takribani miezi 3 iliyopita.
Akizungumza kwenye shoo ya Oga Obinna, Rachel Otuoma alisema
kwamba ahadi na kiapo chake cha kutoivua pete yao ya ndoa bado ingalipo, kwani
hiyo ndio humpa ukumbusho wa kila kitu kizuri Otuoma alimfanyia enzi za uhai
wake.
Pia alikariri kwamba hatoweza badili jina kwa kufuta lile la
Otuoma katika utambulisho wake, akisema kuwa jina hilo limejinafasi katika
sehemu ya upekee kwenye moyo wake.
“Jina Rachel Otuoma
halitawahi badilika. Litakuwa jina langu la matumizi kwa muda wote wa maisha
yangu. Otuoma mwenyewe alinipa jina hilo na mpaka anakufa, sikuwa mtalaka. Hakuna
mahali popote niliandika kwamba mimi ni mtalaka, sema tu kifo ndicho
kilitutenganisha hivyo sioni sababu ya kufuta jina lake,” Otuoma Rachel
alijieleza.
Kuhusu kusonga mbele na maisha na kutafuta mpenzi mwingine,
Rachel aliweka wazi kwamba ingawa uwezekano wa kupenda tena upo, lakini
hafikirii kuingia katika uhusiano serious.
Alisema kwamba huenda akalazimika kuchagua mahusiano ya muda
tu lakini suala la kuingia katika uhusiano wa kudumu ni kibarua kigumu
kuushawishi moyo wake.
“Sidhani kama nitakuwa
katika uhusiano wa kudumu tena, ni mahusiano wazi tu kwa sababu mwanamume wangu
[Otuoma] atasalia daima katika moyo wangu na hii pete yake sitawahi ivua maana
italeta shida,” Rachel alifafanua.
Pia alisimama kidete na kutetea uamuzi wake wa kuhama katika
nyumba ambayo alikuwa akiishi pamoja na marehemu mume wake.
Kulingana naye, asingeweza kustahimili kuendelea kuishi
katika nyumba ile kwa kile akitaja kuwa ilikuwa imejawa na kumbukumbu nyingi za
nyakati zao pamoja hivyo hangeweza kupona kutokana na kifo cha mumewe.
Aliondoka ili kuzikwepa baadhi ya kumbukumbu hizo ambazo
zingechelewesha safari yake ya kupona na kukubali kwamba Otuoma hatokuwepo
maishani naye tena.
“Kulikuwa na kumbukumbu nyingi katika ile nyumba, hivyo
nilifanya uamuzi wa kuhama ili nianze tena upya,” Rachel alisema.
Otuoma alifariki mwaka jana siku chache kuelekea Krismasi na
kuzikwa Mapema januari baada ya kupambana na ugonjwa uliopooza neva zake za
mwili kwa takribani miaka mitano.