
NURU Okanga ametoa wito kwa mbunge wa Kapseret Oscar Sudi kumalizia kumlipa deni la ahadi aliyompa mwaka jana.
Wawili hao walikutana kwenye Obinna Show ambapo Sudi aliahidi
kumpa Okanga shilingi milioni 1.3 kwa ajili ya kufungua biashara.
Akizungumza katika mazungumzo na kituo kimoja cha redio humu
nchini siku chache zilizopita, Okanga alikiri kwamba Sudi alitimiza ahadi hiyo
japo kwa nusu.
Okanga alilaumu vyombo vya habari kwa kuchangia kutopewa
ahadi yote ya Sh1.3 na kupewa Sh700k pekee, kwani Sudi aligoma kumalizia deni
hilo baada ya Okanga kulizungumzia kwa wanahabari.
“Oscar Sudi alinipa
Sh700k taslimu na mimi namheshimu. Lakini unajua watu wa media ndio walizua cheche
wakati waliniuliza kuhusu salio. Nikijibu inaonekana ni makosa. Salio sikupewa,
na huo ndio ukweli wa mambo,” Nuru Okanga alisema.
Hata hivyo, alimtaka Sudi kutii ahadi yake ya kumalizia salio
lililobaki kutoka kwa Sh1.3m kwani ahadi hiyo aliiweka hadharani na kila mtu
akasikia na kuona.
“Nilipewa Sh700k na
niliridhika, lakini maelewano yalikuwa Sh1.3m, na kwa sababu uliweka
makubaliano mbele ya Wakenya, mbona usitimize?” Okanga alimwambia Sudi.
Hata hivyo, kando na kulaumu wanahabari kwa kile alidai ni
kuchonganisha uhusiano wake na Sudi, pia alisema kuwa huenda yeye mwenyewe ni
wa kulaumiwa kutokana na cheche zake dhidi ya serikali.
Okanga alisema kwamba Sudi alivuta nyuma kidogo kumalizia
Sh600k zenye zilikuwa zimebaki kutoka kwa ahadi hiyo baada ya kuona kwamba
anaishambulia serikali.
Ikumbukwe Oscar Sudi ni mwandani na mtetezi mkali wa serikali
ya rais William Ruto ambayo Nuru Okanga amekuwa akiishambulia na kuikosoa bila
kusita.
“Salio lilikuwa limebaki
Sh600k na hayo maneno wakati aliona nimedinda kuunga serikali mkono, ni kama
aliruka makubaliano,” Okanga alisema.
Kuhusu alichofanyia Sh700k alizopokea, Okanga alisema
zilimsaidia kwa njia kubwa kwani aliweka mradi mkubwa wa kujikimu kibiashara
nyumbani kwao, Kakamega.
“Nilienda nyumbani
nikafanya vitu vingi, nilinunua poshomill, nikalipia watoto wengine karo ya
shule, nikaweka mradi wa ufugaji wa kuku, nikakodisha shamba kidogo kidogo
nimepanda mahindi, na miwa…” alieleza.