
MSANII Jose Chameleone kutoka Uganda amefichua kwamba ameacha matumizi ya pombe na sigara, si tu kwa sababu ya kukatazwa na madaktari lakini kwa sababu ya tathmini ya kikweli kuhusu afya yake.
Akizungumza na waandishi wa habari za burudani nchini Kenya
alipotua katika angatua ya JKIA, Chameleone Alifichua kwamba ujio wake Kenya ni
kwa ajili ya matibabu lakini pia kuwasalimia marafiki zake wa muda mrefu.
Msanii huyo ambaye amerudi Afrika kutoka Marekani alikokuwa
akipokea msururu wa matibabu Alifichua kwamba amelazimika kuangalia upya
mienendo ya afya yake bila hata kushauriwa na madaktari.
“Kabla niondoke kwenye
USA nilikuwa nimepoteza takribani kilo 13. Na madaktari hawakunishauri
nisifanye chochote, lakini nilitumia tathmini ya Kibinafsi.”
“Kuna baadhi ya vitu
ambavyo sijakuwa nikifanya vizuri kwa afya yangu. Namaanisha nimekuwa
nikimimina chupa mwilini mwangu, nimekuwa mvutaji sigara maisha yangu yote. Lakini
kwa ajili ya kuboresha afya yangu nimesitisha hivyo vyote. Sasa hivi sivuti
sigara wala sinywi pombe,” Chameleone alieleza.
Msanii huyo ambaye alinusurika kufa alieleza bayana kwamba
aliona wazi Mungu akimpa nafasi nyingine ya kujirekebisha kimaisha na
halichukulii hilo kwa wepesi.
“Hii ni raundi ya pili,
Mungu amenipa awamu. Ya awali ilikuwa ya kwanza na sasa ninaanza ya pili. Na kumbuka
nimesalia na miaka 3 kufikisha miaka 50, hivyo kuna baadhi ya vitu sharti
nivipunguzie kasi,” Chameleone alisema.
Kuhusu kuendelea kimuziki, Chameleone alisema kwamba japo
hajarudi kikamilifu katika maisha yake ya sanaa, bado ana uchu wa kuendelea
ikiwa ni pamoja na kuwashika wasanii wengine mikono.
Msanii huyo ambaye taaluma yake ya muziki ilianzia Kenya
takribani miaka 25 iliyopita Alifichua kwamba Kenya ina maana kubwa kwake kwani
hata mpenzi wake wa kwanza alimpata akiwa Kenya.
Alitoa wito kwa msanii yeyote ambaye anahisi kazi yake ya
muziki ni nzuri na angependa kufanya kazi ya kikoa na yeye kuwasiliana naye
wakati huu ambapo yuko Kenya.
“Watu wengi hawajui
lakini hata mpenzi wangu wa kwanza nilimpata nikiwa hapa Kenya. Vitu vingi
sasna vilitokea kwangu kwa mara ya kwanza nikiwa Kenya, kutoka muziki hadi kila
kitu.”
“Mimi ni hitmaker na kila
mtu anajua hilo. Hivyo nini kingine ninaweza kufanya? Ni wakati wa kuwashika
mikono watu wengine. Siko katika haraka ya kutoa hits, nimeshafanya hivyo kwa
miaka mingi. Mimi naamini katika falsafa kwamba mwangaza wangu kusaidia wengine
kupata nuru hakufifishi wangu,” alisema akikaribisha wasanii kumtafuta
kufanya kazi.