
MSANII mkongwe wa tasnia ya kizazi kipya kutoka Uganda, Jose Chameleone amevunja kimya chake baada ya kurudi nyumbani akitokea hospitalini.
Msanii huyo amekuwa akipokea matibabu katika hospitali moja
nchini Marekani kwa miezi kadhaa na wikendi iliyopita, alirejea nyumbani ambapo
alilakiwa kwa shangwe na nderemo kutoka kwa familia na mashabiki wa muziki
wake.
Chameleone kupitia Instagram yake, alianza kwak umshukuru
Mungu huku akitangaza mabadiliko mapya ambayo ataanza kuyazingatia ili asije
akarudi katika njia ya kulazwa hospitalini tena.
Kulingana naye, sasa na kwenda mbele atakuwa mwangalifu zaidi
haswa katika suala la afya yake lakini pia atapunguza mafadhaiko na pia
kuwaahidi mashabiki wake ujio wa miziki mingi mizuri kutoka kwake.
“Ahsante Mungu tumepita
mabaya. Njia yangu mpya ni kuishi kwa afya. Bila mafadhaiko na kutengeneza
muziki mwingi mzuri,” Chameleone aliandika.
Awali akizungumza na waandishi wa habari, Chameleone Alifichua
kwamba licha ya kurejea nyumbani baada ya kulazwa kwa miezi 4, bado atakuwa
anarejea Marekani kwa matibabu ya mara kwa mara.
Mwimbaji huyo alifichua hayo muda mfupi baada ya kurejea
nchini Uganda, kufuatia kukaa kwa miezi minne nje ya nchi ambako alikuwa
akipatiwa uangalizi maalumu.
Hata hivyo, alikiri kwamba bado hajapona kabisa.
"Bado sijapona…
sijapona kabisa," aliwaambia wanahabari. "Nimerudi kwa sababu
nilitamani nyumbani na nilihitaji kuwa hapa, lakini nitarejea Marekani karibu
Mei 2 kwa ukaguzi."
Katika kikao hicho na wanahabari, Chameleone pia alikanusha
uvumi kwamba afya yake ilikuwa na matatizo kutokana na unywaji wa pombe.
"Kuna idadi ya
mambo, ikiwa ni pamoja na dhiki, DNA (genetics), na ukosefu wa usingizi," alifunguka.