
Msanii mashuhuri kutoka Uganda Joseph Mayanja almaarufu Jose Chameleone, amepelekwa hospitalini kwa dharura nchini Marekani baada ya afya yake kuzorota tena, miezi michache tu baada ya kuondoka hospitalini kufuatia matatizo ya kiafya yanayohusiana na kongosho.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na vyanzo vya karibu na familia yake, Chameleone, alikumbwa na matatizo makali ya kiafya hivi majuzi, hali iliyolazimu apelekwe haraka hospitalini kwa matibabu zaidi.
Mwimbaji huyo mahiri alilazwa kwa mara ya kwanza Desemba 2024 katika Hospitali ya Nakasero jijini Kampala, ambapo alikaa kwa takriban siku 11 akipokea matibabu.
Hali yake ilipoonekana kuwa mbaya zaidi, serikali ya Uganda, chini ya Rais Yoweri Museveni, iliingilia kati na kugharamia safari yake ya matibabu nchini Marekani.
Baada ya muda wa matibabu katika jimbo la Boston, Marekani, alionekana kupata nafuu, lakini mashabiki wake walibaki na wasiwasi kuhusu hali yake ya kiafya.
Hata hivyo, hali hiyo imebadilika ghafla, na msanii huyo amelazimika kurejea hospitalini kwa uangalizi maalum.
Taarifa za kuzorota kwa afya ya Chameleone zimezua mshtuko miongoni mwa mashabiki wake, huku wengi wao wakitumia mitandao ya kijamii kutuma jumbe za faraja na maombi kwa ajili ya kupona kwake.
Familia yake bado haijatoa taarifa rasmi kuhusu hali yake ya sasa, lakini vyanzo vya karibu vinasema madaktari wanafanya kila juhudi kuhakikisha anapata huduma bora za matibabu.
Ndugu wa msanii huyo pamoja na marafiki zake wa karibu wamesisitiza kuwa bado wanahifadhi matumaini kuwa atarejea katika hali yake ya kawaida na kuendelea na maisha yake ya sanaa.
Jose Chameleone ni mmoja wa wasanii wenye ushawishi mkubwa barani Afrika, haswa Afrika Mashariki, akiwa na zaidi ya miongo miwili katika tasnia ya muziki.
Nyimbo zake kama Valu Valu, Badilisha na Wale Wale zimevuma ndani na nje ya mipaka ya Uganda, zikimpatia sifa kama msanii wa kimataifa.
Kwa sasa, mashabiki wake wanasubiri kwa hamu taarifa rasmi kutoka kwa familia yake kuhusu hali yake ya afya, huku wengi wakiendelea kumuombea apate nafuu haraka.