
Msanii maarufu wa Uganda, Jose Chameleone, amekanusha vikali uvumi unaodai kuwa amefungwa gerezani, akibainisha kuwa yuko hospitalini kwa ajili ya upasuaji muhimu.
Haya yanajiri baada ya video ya mwanadada akidai kwamba msanii huyo amefungwa gerezani kusambazwa mitandaoni.
Kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii siku ya Jumanne jioni, Chameleone, ambaye jina lake halisi ni Joseph Mayanja, aliwashukuru mashabiki wake kwa upendo na maombi yao wakati wa kipindi kigumu anachopitia.
Pia alieleza kusikitishwa na video inayosambaa ikidai kuwa amefungwa, akisema:
"Ninawashukuru nyote kwa upendo na maombi yenu. Nimeona video ya mwanadada mmoja mdogo akisema uongo kuhusu mimi kuwa jela n.k. Watu wa aina hiyo wana mawazo gani, hata hivyo? Niko hapa kwa ajili ya upasuaji wangu na nitawajulisha maendeleo yangu. Asanteni watu wangu," Chameleone alisema.
Aliambatanisha ujumbe wake na video iliyomuonyesha akiongea huku akiwa amelala katika kitanda cha hospitali.
Chameleone amekuwa akipambana na matatizo ya kiafya kwa muda.
Mwezi Desemba 2024, alilazwa katika Hospitali ya Nakasero jijini Kampala kwa siku 11 kutokana na matatizo ya kongosho.
Baadaye, alisafirishwa kwenda Hospitali ya Allina Health Mercy nchini Marekani kwa matibabu zaidi, safari iliyogharamiwa na serikali ya Uganda chini ya Rais Yoweri Museveni.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa baba yake, Gerald Mayanja, Chameleone alizidiwa na kukimbizwa hospitalini Massachusetts baada ya kuzimia asubuhi ya Jumanne, Februari 18, 2025.
Rafiki yake, Juliet Zawedde, alithibitisha kuwa msanii huyo anatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa mapafu na kongosho.
Zawedde aliandika kwenye mitandao ya kijamii: "Rafiki yangu kipenzi hajisikii vizuri leo. Amepelekwa hospitalini. Naomba kwa ajili yako, rafiki yangu mpendwa Chameleone. Najua kwa sasa hujisikii vizuri. Bwana akupe mguso wa uponyaji, arejeshe afya na nguvu zako, akufariji katika maumivu yako, na akupe ujasiri wa kukabiliana na changamoto hii."
Familia na mashabiki wa Chameleone wanaendelea kumuombea apate nafuu haraka. Baba yake alieleza: "Chameleone alipaswa kufanyiwa upasuaji mapema, lakini uliahirishwa ili madaktari wafanye vipimo kuhakikisha mwili wake uko tayari kwa upasuaji. Walichunguza moyo wake, shinikizo la damu, macho, na aina ya damu kabla ya kuendelea, kama taratibu zinavyotaka."
Kwa sasa, mashabiki na wapendwa wa Chameleone wanasubiri taarifa zaidi kuhusu maendeleo yake, wakitumaini atapona na kurejea kwenye jukwaa la muziki hivi karibuni.