
ISAAC Otesa maarufu kama Goliath wa Bungoma kwa mara ya kwanza amefunguka kuhusu maisha yake ya kabla ya umaarufu.
Akizungumza kwenye runinga ya TV47 na Dr Ofweneke, Otesa Alifichua
kwamba kabla ya umaarufu wa ghafla shukrani kwa Maandamano ya vijana wa Gen Z,
alikuwa anahangaika na maisha ya kijijini.
Baba huyo wa watoto 3 mwenye umri wa miaka 29 alieleza kwamba
maisha yake ya utotoni hayakuwa rahisi kwani alilazimika kuachia shule katika
darasa la 4 kutokana na kukosekana kwa karo.
Baada ya kuacha shule, Otesa alianza vibarua vya kuchoma
makaa na baadae akajitosa katika biashara ya usafiri wa umma kwa kutumia
bodaboda.
“Karo ilileta shida
nikaachia tu darasa la nne. Kutoka hapo nikaanza kuchimba miti ya kuchoma
makaa, nikaanza kujituma katika vibarua vingine kama kuchungia watu ng’ombe,” Otesa alisema.
Hata hivyo, katika biashara ya bodaboda, alipatwa na majanga
wakati pikipiki aliyekuwa ameichukua kwa mkopo ilipopotea katika mazingira
tatanishi kumpelekea yeye kufungwa jela.
“Baadae niliingia kwa
pikipiki ya mtu nikaanza kumuendeshea pole pole kisha nikaingia kwa chama
nikachukua mkopo. Baadae ile pikipiki ilikuja ikapotea nikashikwa nikafungwa
jela kwa kipindi cha mwezi mmoja,” Otesa Alifichua.
Baada ya kesi kukamilika, alirudi uraiani na kuanza maisha
upya kwa kuendesha pikipiki ya mtu mwingine tena.
“Mungu alinisaidia ile
kesi ikakamilika sikufungwa tena, nikitoka Mungu akafungua njia nikapata
pikipiki ya mtu tena na hivyo hivyo hadi pale hizi harakati za Gen Z zilipoanza
na nikajipata kwenye mwanga wa umma,” Isaac Otesa alisema.
Alisema kwamba hakujua kwamba kuna jamaa mwingine – Bradley Marongo
– ambaye walikuwa na mfanano kama riale kwa ya pili.
Kulingana naye, wakati Bradley alionekana Nairobi kwenye Maandamano,
yeye alikuwa Bungoma akijishughulisha na biashara ya pikipiki wakati polisi wa Trafiki
mmoja alimdokezea kwamba ameona mtu kama yeye Nairobi.
“Mimi niko Bungoma,
ikasemekana kwamba niko Maandamano Nairobi, mimi nikasema sio mimi lakini vile
ilitokea hivyo, mtu mmoja akakuja akasema haya mambo twende Nairobi runingani
tujue ukweli ni upi.”
Hata hivyo, baada ya kufika Nairobi, hakupelekwa runingani
bali alijikuta amepelekwa kwa sosholaiti Manzi wa Kibera akatambulishwa kwa
masuala ya kurekodi video.