Hamisa mnamo siku ya Jumamosi alilipiwa mahari ya ng'ombe 30 na mume wake mtarajiwa, Stephanie Aziz Ki.
Hamisa alionekana kuzidiwa na hisia na hata kutoa machozi ya furaha wakati watoto wake wawili.
Aziz Ki na Hamisa Mobetto
Mwanamitindo maarufu wa Tanzania Hamisa Mobetto mnamo siku ya Jumamosi alilipiwa mahari ya ng'ombe 30 na mume wake mtarajiwa, Stephanie Aziz Ki.
Mshambuliaji huyo wa Yanga SC na raia wa Burkina Faso aliwasilisha ng’ombe hao kwa kutumia lori mbili, hatua hii ikionyesha kuwa mipango ya ndoa yao inaendelea kwa kasi.
Mahari hiyo ilikabidhiwa rasmi kwa familia ya Bi. Harusi na Rais wa Klabu ya Yanga, Hersi Said, kwa niaba ya familia ya Aziz Ki, kwenye hafla maalum iliyofanyika katika Viwanja vya Gofu, Mikocheni, jijini Dar es Salaam.
Katika hafla hiyo, Aziz Ki aliandamana na baadhi ya wachezaji wa Yanga, wakiwemo Pacome Zouzoua, Bakari Mwamnyeto, Yao Kouassi, pamoja na Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ali Kamwe.
Kwa upande wake, Hamisa Mobetto aliwasili eneo la tukio akiwa ameongozana na meneja wake, Paul Mangoma, huku akitanguliwa na warembo 15 waliovalia sare maalum.
Wakati wa hafla hiyo, Hamisa Mobetto alisema anamshukuru Mungu kwa kumpa mpenzi anayemuona kuwa ndiye sahihi kwake na sasa rasmi ni mchumba wa mtu anayempenda kwa dhati.
"Sasa hapa ndipo nimefika, kwa kuwa nimekutana na mtu mwenye mapenzi ya kweli kwangu. Pia, nafsi zetu zimeendana. Namuomba Mungu anyooshe mambo yaende kama tulivyopanga," Hamisa aliambia Mwanaspoti.
Naye Aziz Ki alisema anaamini safari yake ya muda mrefu ya kutafuta mke imefikia mwisho, kwani amempata mwanamke anayempenda kutoka ndani ya moyo wake.
"Taratibu zote za uchumba nimekamilisha. Kilichobaki sasa ni ndoa tu, ambayo itafungwa kesho, Jumapili, Februari 16, 2025. Sherehe rasmi inatarajiwa kufanyika Februari 19, 2025, katika ukumbi wa The SuperDome, Masaki, jijini Dar es Salaam," alisema Aziz Ki.
Hamisa ambaye ni mama wa watoto wawili alionekana kuzidiwa na hisia mara kwa mara wakati wa hafla hiyo, ishara kwamba anafurahia na kutazamia sana kufunga ndoa na Aziz.
Katika video moja kutoka kwa hafla hiyo, mpenzi huyo wa zamani alionekana kuzidiwa na hisia na hata kutoa machozi ya furaha wakati watoto wake wawili, Dylan Abdul Naseeb na Fantasy Majizzo wakimkumbatia yeye na Aziz.
Hamisa pia alionekana kuzidiwa na hisia tena wakati akivishwa pete ya uchumba na mumewe huyo mtarajiwa.