Ibraah wa Konde Gang achukua nafasi ya Harmonize na kutangaza vita na Diamond

"Hapa Dar es Salaam Tanzania eti akae yeye mwaka mzima, hakuna. Sijawahi kumuona, hajawahi tokea na hatawahi kutokea,” Ibraah alisema.

Muhtasari

• Mapema mwezi Julai, Diamond alisema kwamba alikuwa tayari kwa kuachilia kile alichokiita mvua ya mawe,.

• Ibraah amekanusha hilo akisema kwamba Diamond hana uwezo wa kushikilia trendi za muziki kwa mwaka mzima.

Ibraah na Diamond.
Ibraah na Diamond.
Image: Insta

Ibraah, msanii aliyesalijiwa katika lebo ya Konde Music Worldwide inayomilikiwa na msanii mwenza Harmonize ametangaza vita dhidi ya Diamond Platnumz kutoka WCB Wasafi.

Katika mahojiano na waandishi wa habari za mitandaoni akisukuma wimbo wake mpya wa Hapa, Ibraah alisema waziwazi kwamba huu mwezi wa Septemba ni wake kutrendi kwenye namba moja kwenye majukwaa ya kupakua miziki wala hakuna msanii atakayemdungua kwenye namba moja.

Msanii huyo pia alipiga chini kauli ya Diamond kwamba angeshikilia namba moja kwenye trend kwa mwaka mzima pasi na kuwapa wasanii wengine nafasi ya kuonja nafasi ya kwanza kwenye trendi.

Ibraah alisema kwamba tangu aanze muziki, hajawahi ona msanii yeyote wa Tanzania ambaye amekaa namba moja kwenye trendi kwa mwaka mmoja bila kudunguliwa na wala hakuna msanii kama huyo atawahi tokea.

“Huu mwezi ni mwezi wangu, anayejiona yuko sawa tuweke tuweke tuondoke. Kama unaona wewe ni msanii na uko sawa tia chupa nitie chupa tuondoke, eeh. Huu ni mwezi wangu,” alisema.

“Sijawahi kuona huyo msanii na hajawahi zaliwa msanii wa kukaa kwenye trendi namba moja mwaka mzima. Hapa Dar es Salaam Tanzania eti akae yeye mwaka mzima, hakuna. Sijawahi kumuona, hajawahi tokea na hatawahi kutokea,” Ibraah alisema.

Mapema mwezi Julai, Diamond alisema kwamba alikuwa tayari kwa kuachilia kile alichokiita mvua ya mawe, kushikilia kwenye trendi hadi Januari mwakani atakapotoa nafasi kwa wasanii wapya ambao aliahidi atawasaini WCB Wasafi.

Tangu hapo, wasanii wengi wamecharuka kila mmoja akijitia hamnazo kumdungua kutoka namba moja na wengi wameweza kufanikiwa katka hilo.

Kwa upande wake, Ibraah mara kwa mara amekuwa akionekana kuingilia ugomvi unaoendelea baina ya bosi wake Harmonize na Diamond.

Itakumbukwa Harmonize na Diamond walikuwa ni marafiki wakubwa enzi hizo ambapo Diamond ndiye alimshika Harmonize mkono lakini yakaja yakajaa na kupwa baada ya msanii huyo kufaulu.

Tangu kuondoka WCB Wasafi mwishoni mwa mwaka 2019, alianzisha lebo yake ya Konde Music Worldwide ambapo msanii wa kwanza kumpa mkataba alikuwa Ibraah ambaye anatokea huko kwao Mtwara pia.