Msanii wa nyimbo za Mugithi na Gengetone Peter Mwangi almaarufu Miracle Baby ameelezea majuto yake na kuomba msamaha baada ya kushindwa kutimiza ahadi yake kwa Mungu ya kubadili njia na kuhubiri neno lake kwa ulimwengu.
Katika chapisho la Jumapili asubuhi, mtangazaji huyo wa zamani wa TV ambaye miezi kadhaa iliyopita alipambana na ugonjwa mbaya ambao ulimwona akifanyiwa upasuaji mara kadhaa alikiri kwamba alimkosea Mungu kwa kuvunja ahadi yake Kwake.
Miracle Baby alikiri jinsi Mungu alivyomuokoa kutoka katika hali mbaya ambayo alijikuta nayo na akamuomba msamaha.
"Mungu tafadhali nisamehe, NAJUA nimehaibisha Kazi yenye ulinifanyia nikiwa sina matumaini ya kuwahi ISHI TENA hii DUNIA,” Miracle Baby alisema kupitia Instagram.
“NAJUA nimesahau KWENYE ulikuwa umeniambia NIENDE kwa watu wasio na matumaini na WENYE walikuwa na kiu ya kukujua, badala niwafikishie niliingiwa na kiburi na kujiona najua saana, tafadhali nisamehe Mungu kwa hilo����,” aliongeza.
Mwimbaji huyo alikiri kuwa hawezi kufanya lolote bila Mungu na akamwomba Muumba amhurumie na amsamehe kwa kuteleza.
Aliendelea kumwomba Mungu amwongoze anapochagua kutembea katika njia ya utakatifu.
.“BWANA, nimefanya dhambi. Bila neema Yako, mimi hupungukiwa kila wakati. Wewe ni mwaminifu wa kunisamehe na kunitakasa. Nataka kutembea katika haki na utakatifu, lakini nahitaji msaada wako!������,” alisema.
Haya yanajiri siku chache tu baada ya mwimbaji huyo kuonekana akitumbuiza wapenda burudani katika eneo la burudani licha ya kutangaza mapema kuwa ameamua kuwa mchungaji.
Awali mwezi Juni, mwimbaji wa Gengetone alifurahisha mashabiki wake kwa uamuzi wake wa kuwa mchungaji. Hii ilikuja baada ya matatizo ya kiafya.
Alitangaza kwamba alikuwa katika safari ya kujitafutia mwenyewe alipokuwa ameketi kwenye mimbari na Mchungaji mzee.
Tangu wakati huo, amekuwa akiimba nyimbo nyingi za injili za Kikuyu, na katika baadhi ya matukio ameshirikiana na aliyekuwa mkewe Carol Katrue.