logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Mbosso Azungumzia Kufungua Lebo Baada Ya Kuondoka WCB, Uhusiano Wa Sasa Na Diamond

Mbosso aliondoka WCB mwezi jana baada ya kuwa chini ya lebo hiyo inayoongozwa na Diamond tangu mwaka 2018.

image
na Samuel Mainajournalist

Mastaa wako20 February 2025 - 10:58

Muhtasari


  • Mbosso ametoa shukrani zake kwa Diamond, akisema kuwa ni tendo la upendo na ukarimu mkubwa kwa yeye kumruhusu aondoke bila masharti.
  • Mtunzi huyo wa kibao ‘Hodari’ alisisitiza kuwa, licha ya kuondoka WCB, uhusiano wake na Diamond bado uko imara.

Diamond na Mbosso jukwaani

Staa wa Bongo Mbwana Yusuf Kilungi almaarufu Mbosso Khan amethibitisha rasmi kuondoka katika lebo ya muziki ya WCB.

Akizungumza katika mahojiano na Ayo TV, msanii huyo ambaye amekuwa chini ya lebo hiyo ya Diamond Platnumz kwa takriban miaka saba alithibitisha kuwa hakupewa masharti ya kulipa chochote ili kuondoka.

Mbosso alieleza shukrani zake kwa Diamond, akisema kuwa ni tendo la upendo na ukarimu mkubwa kwa bosi wake wa zamani kumruhusu aondoke bila masharti. Alimshukuru pia kwa kubariki uamuzi wake wa kuondoka na akaweka wazi kuwa wataendelea kushirikiana.

"Kama alivyozungumza (Diamond), ni jambo la baraka, ni jambo ambalo ndani yake lina upendo mkubwa sana. Kuna baadhi ya vitu ambavyo pesa huenda zisiweze kununua kama upendo na namna ambavyo tumeishi. Pengine hata ningelipa pesa, kwa sababu nilikuwa tayari kumlipa, lakini huenda pesa ambazo ningelipa hazingetosha hata kufanya service ya gari zake tu, kwa sababu yule tajiri ana pesa nyingi," Mbosso alisema.

"Kwa hiyo hakuona sababu ya mimi kutoa hizo pesa zote kwa namna ambayo tumeishi na tumeshirikiana, na bado tunaendelea kushirikiana kwa njia moja au nyingine," aliongeza.

Mtunzi huyo wa kibao ‘Hodari’ alisisitiza kuwa, licha ya kuondoka WCB, uhusiano wake na Diamond bado uko imara.

Aidha, alikanusha uvumi uliokuwa ukienea mitandaoni kuwa Diamond amekumbwa na mafhaiko baada ya yeye kuondoka, akithibitisha kuwa bosi wake wa zamani yuko salama na anaendelea vyema.

"Sijui niseme namuahidi nini. Ni mtu ambaye nazungumza naye kila siku. Pia anafahamu vitu vingi tunavyozungumza, tunavyosaidiana, tunavyoshirikiana. Bado tunashauriana na tunawasiliana kwa kiwango kikubwa sana. Tunatumiana vitu vingi sana, vichekesho na mambo mengine. Tunaongea vizuri. Anafahamu mimi ni mdogo wake, sina shida naye, na hategemei negativity yoyote kutoka kwangu," alisema.

"Hana msongo wa mawazo, mimi ninavyoongea naye ni vitu vingine. Hayo mambo yanayoenezwa mitandaoni nayaona tu nacheka."

Kuhusu mipango yake ijayo, Mbosso alisema kuwa kwa sasa anapanga kujikita zaidi katika kazi yake ya muziki kabla ya kuingia katika miradi mikubwa zaidi.

Pia alieleza kuwa hana haraka ya kuanzisha lebo yake ya muziki kwa sababu bado hajaweza kufikia kiwango cha kusimamia wasanii wengine.

"Sidhani kama niko na haraka sana ya kuanzisha record label. Nahitaji kwanza kuwadhihirishia Watanzania mambo mengi kabla ya kuanza kusimamia wasanii. Nikisema nakurupuka na kuanzisha lebo halafu nikamchukua msanii na kumharibu, haitakuwa vizuri. Nashuhudia watu wanaanzisha lebo, inafika mahali msanii hajakuwa mzuri na kuna changamoto nyingi. Kwa hiyo sitaki hivyo. Nataka nijizatiti kwanza, nikiona mambo yanaenda vizuri, mengine yatafuata," alisema.

Mbosso aliondoka WCB mwezi uliopita baada ya kuwa chini ya lebo hiyo inayoongozwa na Diamond Platnumz tangu mwaka 2018.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved